Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Licha ya COVID-19 wahudumu walio mstari wa mbele wanasaidia manusura wa usafirishaji haramu- UNODC

Licha ya COVID-19 wahudumu walio mstari wa mbele wanasaidia manusura wa usafirishaji haramu- UNODC

Pakua

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu, Umoja wa Mataifa umepigia chepuo na kuwapongeza wafanyakazi walio mstari wa mbele kusaidia na kunasua watu waliosafirishwa kiharamu hususan wakati huu wa janga la ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19.

Mkurugenzi Mtendaji wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na madawa ya kulevya ya uhalifu, UNODC, Ghada Waly amesema kuwa katika janga la COVID-19, hatari za kusafirishwa kiharamu zimeongezeka akitaja sababu kuwa ni,“Kupotea kwa ajira, ongezeko la umaskini, kufungwa kwa shule na ongezeko la mwingiliano wa watu  kupitia mitandao ya kijamii, mambo ambayo yanaongeza hatari zaidi na kuvipatia fursa vikundi vya uhalifu. Janga hili la COVID-19 limesababisha huduma za kijamii na umma kuzidiwa uwezo, na hivyo kukwamisha mifumo ya sheria na haki na hata kusababisha iwe vigumu kwa manusura wa usafirishaji haramu kusaka msaada.” 

Hata hivyo amesema licha ya nyakati ngumu wakati huu wa COVID-19, wafanyakazi walio mstari wa mbele kusaidia manusura wameweka maisha yao rehani, na wao UNODC wanawaunga mkono, "Kwa kupeleka fedha kusaidia manusura, kuwapatia watendaji wanaokabili usafirishaji haramu malazi na vifaa vya kujikinga, na pia kusaidia nchi wanachama kupunguza makali ya shida zitokanazo na janga la COVID-19 kwenye harakati za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu.” 

Ametoa wito kwa kila mtu kuonesha mshikamano kwa kuunga mkono kampeni ya UNODC ya Moyo wa Buluu dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
1'34"
Photo Credit
World Bank/Peter Kapuscinski