Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakazi wa Mathare nchini Kenya washukuru UNICEF kwa kuwawekea tenki za maji

Wakazi wa Mathare nchini Kenya washukuru UNICEF kwa kuwawekea tenki za maji

Pakua

Maambukizi mapya ya ugonjwa wa virusi vya Corona au COVID-19, yakiendelea kuripotiwa nchini Kenya, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini humo limeanzisha zaidi ya vituo 1000 vya kunawa mikono katika eneo la makazi duni la Mathare kwenye mji mkuu Nairobi, kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi mapya. Loise Wairimu na ripoti kamili.

Eneo hili la Mathare, jijini Nairobi nchini Kenya, lenye zaidi ya wakazi 200,000 [Laki Mbili] ambao uhaba wa maji safi na salama kwenye eneo hilo ni mwiba katika kutokomeza COVID-19.

UNICEF kwa kutambua hilo ilishirikiana na wadau ambao serikali ya jiji la Nairobi na shirika la misaada la Uingereza, UK Aid na kufunga vitu hivyo vya kunawa mikono vyenye maji safi na sabuni.

Ally Tifow ni mtaalamu wa Maji, Huduma za Kujisafi au WASH, UNICEF Kenya na anasema kuwa,

“Huduma hizi ni muhimu katika kuzuia COVID-19, kwa kuzingatia wakazi wa maeneo haya hawana huduma za maji safi na kujisafi. Hapa nchini na hasa vitongoji duni vya mijini kama Nairobi, havina huduma za maji salama.”

Miongoni mwa wanufaika wa mradi huo ni Mary Mwongeli na binti yake Precious Ng’undu mwenye umri wa miaka 9 ambaye anazungmzia vile ambavyo mama yake anamuelimisha kuhusu COVID-19.

 “Mama amenieleza kuwa ni lazima kila wakati kunawa mikono yetu, na tusiende kwenye maeneo ya umati kwa kuwa hatufahamu ni nani ana Corona. Na hata wewe mwenyewe hufahamu kama una virusi, na kila wakati unapotoka nje uvae barakoa.”

Kwa Mary, tenki hizo za maji ni msaada mkubwa..

“Watu wa UNICEF walikuja wakaleta tenki na kuziweka maeneo ya wazi. Ukitembea tu eneo dogo, unakuta tenki la maji na kuna sabuni, unaweza kunawa mkono na kuondoka.”

Precious, ndoto yake ni kuwa daktari ili aweze kuokoa maisha ya watu na kujenga amani, lakini pia ujumbe,

“Nataka niwaambie watoto hapo mlipo, lazima mnawe mikono na mvae barakoa.”

 

 

Audio Duration
2'15"
Photo Credit
© UN-Habitat /Julius Mwelu