Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

15 Aprili 2020

15 Aprili 2020

Pakua

FLORA NDUCHA : Hujambo na Karibu kusikiliza Jarida kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa, kutoka hapa Marekani.

JINGLE (04”)

FLORA:Ni Jumatano  ya 15 Aprili mwaka 2020, mwenyeji wako hii leo ni mimi FLORA NDUCHA

1: Huu si wakati wa kusitisha ufadhili kwa WHO- Guterres
 
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema huu si wakati wa kupunguza rasilimali za kufanikisha operesheni za shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO. Grace Kaneiya na ripoti kamili.
 
(Taarifa ya Grace Kaneiya)
 
Bwana Guterres amesema hayo katika taarifa iliyotolewa Jumanne usiku na msemaji wake jijini New York, Marekani akisema kuwa siyo tu kwa WHO bali pia si wakati wa kupunguza rasilimali kwa shirika lolote lile la kibinadamu linalopambana hivi sasa na ugonjwa wa virusi vya Corona, COVID-19.
 
Kauli ya Katibu Mkuu imekuja saa chache kufuatia tangazo la leo Jumanne la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha fedha kwa WHO, hadi baada ya tathmini ya hatua za shirika hilo dhidi ya mlipuko wa COVID-19.
 
Katibu Mkuu amerejelea kauli yake ya tarehe 8 mwezi huu ya kwamba janga la COVID-19 ni moja ya changamoto kubwa kuwahi kukumba dunia na ni janga kubwa zaidi la kibinadamu lenye madhara makubwa kijamii na kiuchumi.
 
Amesema maelfu ya wafanyakazi wa WHO wako  mstari wa mbele wakisaidia nchi wanachama na wananchi wao hususan walio hatarini zaidi, wakiwapatia mafunzo, mwongozo, vifaa na huduma muhimu za kuokoa maisha huku wakikabiliana na virusi.
 
 
(sauti ya Antonio Guterres)
 
“Wapendwa janga hili linarejesha nyumbani umoja wetu ambao ni muhimu katika familia ya ubinadamu wetu. Kuzuia kuenea zaidi kwa COVID-19 ni jukumu letu zote kwa pamoja. Umoja wa Mataifa likiwemo shirika la afya duniani umejipanga kikamilifu.Kama sehemu ya familia yetu ya kibinadamu tunafanya kazi saa 24 siku 7 kwa wiki na serikali ili kutoa muongozo wa kimataifa kuusaidia ulimwengu kuchukua hatua za kukabili tishio hili.”
 
Guterres amesema ni kwa imani yake kuwa WHO inapaswa kuungwa mkono kwa sababu bila shaka ni muhimu sana katika juhudi za dunia za kupambana na COVID-19.
 
Amesisitiza kuwa huu ni wakati wa mshikamano na wakati wa umoja na jamii ya kimataifa kushirikiana na kukomesha hivi virusi na madhara yake.


===================================================

2: Watoto wako katika hatari zaidi ya kuathiriwa na muda mwingi mitandaoni wakati huu wa COVID-19-UNICEF
 
Mamilioni ya watoto wako hatarini kudhurika wakati huu ambao maisha yao yamehamia zaidi mitandaoni wakati wa kukaa ndani kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19, imeeleza taarifa iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF pamoja na wadau wake. Jason Nyakundi na maelezo zaidi
 
(Taarifa ya Jason Nyakundi)
 
UNICEF na wadau wake ambao ni Global Partnership to End Violence Against Children ambayo ni taasisi ya kutokomeza unyanyasaji dhidi ya watoto, shirika la kimataifa la muungano wa mawasiliano, ITU, Shirika la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO, ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na madawa na uhalifu UNODC, WHO, WePROTECT Global Alliance na World Childhood Foundation wametoa waraka unaolenga kuzisihi serikali, tasnia ya mawasiliano, watoa elimu pamoja na wazazi kuwa makini na kuchukua hatua za kupunguza hatari na kuhakikisha uzoefu wa watoto mitandaoni unakuwa salama na unatoa mchango chanya wakati huu wa COVID-19.
 
Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Henrietta Fore (tamka /fôr/ kama 4) amesema, “katika kivuli cha COVID-19, maisha ya mamilioni ya watoto kwa muda yamejikita katika nyumba zao na vifaa vyao vya kielekroniki. Tunatakiwa kuwasaidia kupita katika ukweli huu mpya. Tunatoa wito kwa serikali na tasnia kuunganisha nguvu kuwaweka watoto salama mitandaoni kupitia huduma zilizoboreshwa na zana mpya za kuwasaidia wazazi na watoa elimu kuwafundisha watoto wao jinsi ya kutumia intaneti kwa usalama.”
 
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Global Partnership to End Violence akilisisitiza suala hilo anasema, “kusambaa kwa virusi cha corona kumesababisha kuongezeka kwa kasi kwa muda wa kuangalia vifaa vya kielekroniki. Kufungwa kwa shule pamoja na hatua kali za kuudhibiti ugonjwa vinamaanisha familia kutegemea zaidi kwenye teknolojia na dijitali ili kuwafanya watoto wajifunze, kuburudika na kuungana na watu waliko nje ya mazingira yao, lakini si wote wana uelewa, ujuzi na rasilimali za kujiweka salama wawapo mitandaoni.”
 
Taarifa hiyo ya UNICEF inaendelea kusema kuwa zaidi ya watoto na watu bilioni 1.5 pamoja na watu wengine wa umri mdogo wameathirika na kufungwa kwa shule duniani kote. Wengi wa wanafunzi hawa hivi sasa wanapata mafunzo yao pamoja na kuwasiliana na wenzao kupitia mitandaoni.
 
“Kutumia muda mwingi katika mitandao kunaweza kuwaweka watoto katika hatari ya  manyanyaso ya kingono pamoja na kuingizwa katika tabia hizo kwani watu wabaya wanataka kutumia janga hili la COVID-19 kutekeleza mambo mabaya.” Imeeleza taarifa hiyo ya UNICEF.
 
Aidha taarifa hiyo imesema kukosekana kwa fursa ya watoto kukutana ana kwa ana na marafiki na wenzi wao kunaweza kusababisha hatari ya watoto kutumiana picha chafu na pia muda mwingi wa kukaa mtandaoni unaweza kuwafanya watazame maudhui ya vurugu na pia kuwaweka katika uwezekano wa kufanyiwa manyanyaso mtandaoni.

 ====================================================
STUDIO. MIDWAYSTING
====================================================
FLORA: Punde ni makala ambapo tutaelekea nchini Tanzania kusikia ubunifu wa vijana waliounda mashine ya kielektroniki inayotoa huduma ya maji safi na salama. 
====================================================

3: Hakuna mtoto wala mama anayestahili kufa wakati wa kujifungua:UNFPA 
Shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA limesema hakuna mtoto wala mama anayestahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua nchini Haiti na ndio maana limeamua kulivalia njuga tatizo hilo . Tupate maelezo zaidi na John Kibego
 
(TAARIFA YA JOHN KIBEGO)
NATTS……
Huyo ni mmoja wa ndugu wa binti aliyepoteza maisha wakati wa kujifungua mjini Port-au Prince nchini Haiti akisema binamu yale aliyekuwa mjamzito alifia hospitali wakati anajifungua na mwanaye mchanga alikufa pia.
Kwa mujibu wa shirika la UNFPA Haiti ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya vifo vya wakati wa kujifungua vya watoto na kina mama kutokana na sababu mbalimbali lakini kubwa zaidi ni uhaba wa wauguzi na wakunga wenye ujuzi unaohitajika.
Zaidi ya kina mama 500 kati 100,000 hupoteza maisha wakati wakijifungua nchini humo na takriban theluthi mbili hujifungua bila msaada wowote wa muuguzi au mkunga. Stefani Roche ni mkunga katika moja ya hospitani mjini Port-au-Prince
(SAUTI YA STEFANI ROCHE-ASSUMPTA)
“Kuwa na fursa ya kumpata muuguzi na mkunga mwenye ujuzi bado ni changamoto kubwa kwetu kwa sasa. Tunachokitaka ni kwa wanawake kujifungua katika mazingira salama bila hatari.”
Eloniese Vilise ni miongoni mwa kina mama ambaye wakati wa ujauzito wake alihuduria kliniki kwa mkunga Roche katika hospitali hii kila wiki kupata ushauri kuhusu afya yake na lishe na akajifungua salama mtoto wa kike.
(SAUTI YA ELONIESE VILISE-GRACE)
“Ninamambo mazuri tu ya kusema kuhusu mkunga Stefani Roche kutokana na jinsi anavyohudumia na kusaidia watu, nilihisi ni kama rafiki yangu na ndio maana namshukuru sana.”
Kwa kutambua changamoto wa waugunzi na wakunga  na mahitaji nchini Haiti sasa UNFPA inashirikiana na wadau kutatua changamoto hiyo ikisema kupatikana kwa wakunga waliofuzu kunaweza kuokoa maisha ya kina mama 28,000 wakati wa kujifungua kila mwaka.
Miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na shirika hilo ni kutoa mafunzo kwa wauguzi na wakunga, vifaa, kutoa elimu kwa kina mama wajawazito na kuwekeza katika kuongeza idadi ya wahudumu hao muhimu wa afya katika hospitali zikiwemo z vijijini.
 
===================================================
STUDIO: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
FLORA: Na sasa ni wasaa wa makala hii iliyoandaliwa na Nyota Simba pamoja na Evarist Mapesa kuhusu ubunifu wa vijana jijini Mwanza Tanzania waliounda mashine ya kutoa huduma ya maji safi na salama. Msimuliaji ni Nyota Simba.
=================================================
STUDIO: PLAY MAKALA
====================================================

ASSUMPTA: Play MUSIC 4 for 5 seconds and hold under
====================================================
FLORA: Asante sana Nyota Simba na Evarist Mapesa kwa makala hii. 
 ====================================================
Na sasa ni mashinani, mwendazake Ken Walibora mwanariwaya kutoka Kenya alikuwa mchambuzi wetu wa lugha ya Kiswahili, na leo tunakumbuka moja ya simulizi zake.
 ===================================================
Studio: Play Mashinani
====================================================
FLORA: Naam Ken Walibora! Mola akulaze pahala pema peponi Amen.
==================================================
STUDIO: Play Bridge

FLORA: Na hadi hapo natamatisha jarida letu la leo. Tupatane kesho kwa habari na makala kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa unaweza kupata matangazo na taarifa nyingine na kujifunza Kiswahili kwenye wavuti wetu news.un.org/sw. Msimamizi  wa matangazo ni ASSUMPTA MASSOI na mimi ni FLORA NDUCHA, nasema kwaheri kutoka Marekani.

==================================================
TAPE: CLOSING BAND

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
12'5"