UNMISS yapeleka nuru kwa watoto wa Rumbek, Sudan Kusini

11 Novemba 2019

Walinda amani wanaohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini,  UNMISS wamekamilisha  ujenzi wa moja ya majengo matatu ya madarasa ya shule ya msingi huko eneo la Rumbek, jimbo la Lake na hivyo kuleta matumaini kuwa watoto wengi wa kike wanaweza kuepushwa na ndoa za  mapema. Brenda Mbaitsa na ripoti kamili.

Mjini Rumbek, katikati mwa Sudan Kusini, mafundi waashi wakijenga tofali baada ya tofali ili kurejesha ndoto za watoto hasa wale wa kike.

Baada ya msingi kukamilia, kuta nazo na hatimaye jengo zima na hii ikiashiria kuwa jengo jipya la darasa kwa wanafunzi wa shule ya msingi ya Asementi, limetimiza ndoto zao.

Awali walisomea chini  ya miti ilhali wengine walisomea kwenye jengo bovu.

Akoth Maker, ni kiongozi wa eneo hili la Gok na anasema kuwa “mvua ziliponyesha, watoto walikimbia kutoka chini ya mti na kuingia kwenye darasa bovu kwa kuwa sehemu ya darasa ilishabomoka na tulihofua linaweza kuwaangukia. Kila siku tulijiuliza iwapo tuache watoto kwenye mvua chini ya mti au wajikinge kwenye darasa lililobomoka.”

Nia ya wanafunzi kusoma na walimu kufundisha ilifanya waendelee hivyo hivyo lakini sasa majengo haya matatu yameleta hamasa hata wakati wa makabidhiano.

Ujenzi huu ni sehemu ya miradi ya matokeo ya haraka ya UNMISS na matarajio ni kwamba wanafunzi wengi zaidi wataandikishwa suleni na ndoto ya wazazi kutimia kama asemavyo Caroline Opok, afisa kutoka UNMISS.

 “Tulipofika hapa mara ya kwanza, watoto wengi wa kike walikuwepo hapa uwanjani n ahata kufundishana wenyewe kwa wenyewe. Walio madarasa ya juu wanafundisha walio madarasa ya chini. Na tulipozungumza na wazazi walitueleza kuwa mtoto wa kike anapokuwepo shuleni, kuna fursa ndogo sana ya kuozwa mapema kwa sababu ana muda wa masomo. Kwa hiyo walisema iwapo shule itakuwepo karibuni, watapeleka watoto wengi wa kike shuleni na hawatalazimika kwenda umbali mrefu kwa kuwa wanahofia watoto wao kwenda mbali.”

Watoto waliingia kwenye madarasa mapya wakiwa na ndoto mpya huku mwalimu mkuu wa shule hii ya msingi ya Asementi Majak Marial anasema…

“Hili moja limekamilika na wanafunzi wote wanafika hapa kusoma wakiwa na furaha kwani wana jengo jipya.”

Licha ya mkwamo  uliopo ikiwemo ukosefu wa madaftari, kalamu, penseli na ubao, ndoto ya watoto hawa ya kuwa madaktari, walimu na wanasheria inazidi kuendelea kuimarika.

Audio Credit:
Flora Nducha/Brenda Mbaitsa
Audio Duration:
2'20"

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud