Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO yatiwa hofu na hali ya huduma za afya kaskazini-mashariki mwa Syria, OCHA nayo yazungumza

WHO yatiwa hofu na hali ya huduma za afya kaskazini-mashariki mwa Syria, OCHA nayo yazungumza

Pakua

Shirika la afya duniani kuptia taarifa yake iliyotolewa mjini Cairo Misri, limeonesha wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya afya ya binadamu kaskazini mwa Syria ambako watu takribani 200,000 wameyakimbia makazi yao kutokana na ongezeko la operesheni za kijeshi tangu Oktoba 9 na hivyo watu milioni 1.5 wako katika uhitaji mkubwa wa huduma za kiafya. Taarifa zaidi na Brenda Mbaitsa

WHO imeeleza kuwa hivi sasa watu wapatao milioni 1.5 wako katika uhitaji mkubwa wa huduma za kiafya na wengi wao waliothiriwa na ukatili wa hivi karibuni tayari wamepata msongo mkubwa wa akili na akili ikiwa ni  matokeo ya miaka ya migogoro na kufurushwa mara kwa mara.

WHO imesema, watu walioko katika mahitaji makubwa ya huduma za kiafya wanakabiliana na changamoto zinazohusiana na ukosekanaji wa usalama na ufikiaji mdogo wa huduma za kiafya.

Imeongeza kuwa tayari miundombinu ya huduma za kiafya kaskazini mwa Syria zimeathirika sana kutokana na hali ya kukosekana kwa usalama iliyotokea hivi karibuni.

Hospitali ya taifa ya Al-Ain mjini Ras hivi sasa haitoi huduma na hospital nyingine ya taifa na vituo viwili vya afya mjini Tel Abyad vyote havifanyi kazi.

Vituo vyote vya afya katika kambi vilivyokuwa vinawapokea waliofurushwa Ain Issa na Ras Al Ain pia vimefungwa na watu kuahamishwa kutokana na kuongezeka kwa uwezekano wa kushambuliwa.

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA imeeleza kuwa hali mbaya na watu waliofurushwa wanakadiriwa kufikia kati ya 150,000 hadi 160,000 na ripoti za wengine wanaohama zinazidi kumiminika.

Wakati huo huo kupitia taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake jijini New York, Marekani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ameendelea kuhisi pande  kinzani zijizuie na zitambue kuwa operesheni za kijeshi zinapaswa kuheshimu sheria ya kimataifa ikiwemo Katiba  ya Umoja wa Mataifa na sheria ya kibinadamu ya kimataifa.

Katibu Mkuu ametoa wito wa sitisho la mashambulizi haya mara moja na kusihi pande zote kinzani zisake suluhu kwa njia ya amani.

 

Audio Credit
Assumpta Massoi/Brenda Mbaitsa
Sauti
2'22"
Photo Credit
© OCHA/Hedinn Halldorsson