Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada mvua Bangladesh, sasa maji yatiririka mabondeni, wakazi wahaha, WFP yaendelea kusaidia

Baada mvua Bangladesh, sasa maji yatiririka mabondeni, wakazi wahaha, WFP yaendelea kusaidia

Pakua

Nchini Bangladesh, shirika la mpango wa chakula duniani, WFP linafuatilia hali halisi kufuatia mvua kubwa za pepo za monsuni ambazo zimesababisha mafuriko na ongezeko la kiwango cha maji kwenye mito. Grace Kaneiya na ripoti kamili.

Ni kwenye wilaya ya Cox’s Bazar nchini Bangladesh, eneo ambako ni kambi ya wakimbizi kutoka Myanmar. Pepo za monsuni zimesababisha mafuriko si tu kwenye eneo hilo bali pia katika maeneo mengine ya taifa hili la Bangladesh lenye watu milioni 161 kando ya wakimbizi inaohifadhi.

Msemaji wa WFP mjini Geneva, Uswisi Herve Verhoosel amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa hali ya aina hii na mbaya zaidi ni kwenye wilaya za Kurigram, Gaibandha na Jamalpur ambako viwango vya maji vinazidi kuongezeka.

Amesema kuwa hivi sasa wanashirikiana na wadau, zikiwemo serikali za mitaa na kwa mujibu wa takwimu mpya za serikali jumla ya watu milioni 2.3 wameathiriwa na mvua hizo kwenye vitongoji 115 vya wilaya 20.

Pepo za monsuni zimekuwa na madhara makubwa kila wakati kwa Bangladesh, taifa ambalo lina zaidi ya mito 700 na hivyo kuliweka hatarini na mafuriko pindi mvua hizo zinaponyesha.

WFP inasema pamoja na mafuriko, mabadiliko ya tabianchi nayo yamekuwa ‘mwiba’ kwa Bangladesh kwa kuwa theluji katika miliya ya Himalaya inayeyuka kutokana na ongezeko la kiwango cha joto na hivyo maji ya mito yanatiririka kuelekea taifa hilo.

Bwana Verhoosel ametolea mfano wa wakazi wa wilaya ya Kurigram akisema wao wako hatarini zaidi kwa sababu eneo lao lipo katika kingo za mito na kwamba pindi kuna mafuriko, nyumba zao na ardhi yao ya mashamba na mbinu zao za kujipatia kipato vinasombwa.

Kwa mantiki hiyo amesema ndio maana kwa miongo kadhaa sasa WFP inakuwa mstari wa mbele kuwajengea mnepo wakazi wa nchi hiyo ili waweze kukabiliana na majanga  hayo

Audio Credit
Assumpta Massoi/Grace Kaneiya
Audio Duration
2'2"
Photo Credit
Bangladesh Red Crescent Society/Bandarban Unit