Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen imesaidia sana wakati umefika kuilipa fadhila: UN

Yemen imesaidia sana wakati umefika kuilipa fadhila: UN

Pakua

Jumuiya ya kimataifa imechagizwa kulipa fadhila kwa Yemen ambayo imeelezwa kuwa katika zahima kubwa na janga baya zaidi la kibinadamu duniani, nchi ambayo ambayo awali iliwakarimu wageni, waomba hifadhi na hata wakimbizi, sasa imejikuta njia panda mamilioni ya watu wake wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. 

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mjini Geneva Uswis hii leo kwenye mkutano wa kimataifa wa harambee ya kuchangisha fedha kwa ajili ya usaidizi wa kibinadamu Yemen.

Ameongeza kuwa watu milioni 22 wanahitaji msaada wa kibinadamu na milioni 18 kati yao hawajui hata mlo unaofuata utatoka wapi, hivyo ameihamasisha jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kumaliza madhila kwa watu hao

(SAUTI YA ANTONIO GUTERRES)

“Ninawaomba wote kufanya kila liwezekanalo, ni lazima tuone hatua za kukomesha vita. Vita hivi vinasababisha madhila makubwa ya kibinadamu kwa watu ambao ni masikini kabisa na wasiojiweza duniani. Hakuna suluhu ya kibinadamu kwa mgogoro wa kibinadamu, muafaka wa kisiasa kupitia majadiliano yatakayojumuisha Wayemen wote ndio suluhu pekee.”

 

Amewaasa pia wahisani kuchangia kwa moyo wote kwani usaidizi wa kibinadamu Yemen mwaka huu 2018 unahitaji dola bilioni 2.96 ili kuwafikia watu milioni 13 wenye mahitaji ya haraka nchi nzima.

 

Naye mratibu wa masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Marck Lowcock amesisitiza umuhimu wa fedha zitakazochangishwa kwenye mkutano huo kushughulikia masuala muhimu manne

 

(SAUTI YA MARK LOWCOCK)

Mosi tunahitaji bandari zote Yemen kusalia wazi bila vikwazo vyovyote, pili tunahitaji mishahara yote ya sekta za umma kulipwa ikiwemo kuzuia mlipuko mwingine wa kipindupindu na kuwaweka watoto shuleni. Tatu tunahitaji kupata fursa ya kufika kila pembe ya nchi , nne na la muhimu zaidi tunataka kuona hatua zinapigwa kukomesha vita na pande zote kushirikiana na mwakilishi maalumu kwa ajili ya amani endelevu.”

 

Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa kupiga hatua Yemen na kumaliza vita sio kitu kinachoshindikana isipokuwa itategemea kila mmoja kutimiza wajibu wake.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'16"
Photo Credit
Familia nchini Yemen wapata lishe muhimu mara moja tu kwa siku. Picha: WFP