Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisheni mapigano Syria tufikishe misaada- UN

Sitisheni mapigano Syria tufikishe misaada- UN

Pakua

Nchini Syria hakuna dalili zozote za mapigano kumalizika huku watoto walionasa kwenye mzozo huo wakiendelea kukumbwa na jinamizi kila uchao.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF Henrietta H. Fore katika taarifa yake iliyotolewa New York, Marekani.

Amesema anavunjika moyo kwa kile ambacho watoto wa Syria wameendelea kukabiliana nacho kutokana na vitendo vya watu wazima, vitendo ambavyo amesema vinapuuza kabisa ulinzi, usalama na ustawi wa watoto.

Kw mantiki hiyo amesema UNICEF inaungana na wito wa kimataifa wa kusitisha chuki na mapigano Syria akitaka maeneo ya kijamii kama vile shule, afya na viwanja vya michezo ni lazima yawe salama na yasilengwe.

Naye Panos Moumtzis ambaye ni mratibu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu kwenye ukanda wa Mashariki ya Kati amezungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa akisema misaada ipo lakini shida ni kuifikisha kwenye maeneo yaliyozingira kama vile Idlib, Afrin na Ghouta Mashariki.

Amesema hadi sasa ombi la sitisho la mapigano limegonga mwamba..

(Sauti ya Panos Moumtzis)

“Kwa kweli tunasihi nchi zote zenye ushawisi kutumia shinikizo lolote kutusaidia ili makubaliano ya kisiasa yaweze kutekelezwa na tufikie watu walio kwenye maeneo yasiyofikika. Hadi sasa hatujaona matokeo yoyote lakini tunaendelea kushinikiza kwa njia zote ili tufanikiwe.”

Mapigano nchini Syria yalianza mwaka 2011.

Audio Credit
Taarifa ya Assumpta Massoi
Sauti
1'35"
Photo Credit
UNICEF/Khuder Al-Issa