Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yataka wafuasi wa UDPS DRC waachiwe huru

MONUSCO yataka wafuasi wa UDPS DRC waachiwe huru

Pakua

Ujumbe wa la Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC,  (MONUSCO) umelaani vikali kitendo cha vikosi vya usalama nchini humo kukamata idadi kubwa ya wanachama wa chama cha upinzani cha UDPS, katika mji wa Lubumbashi, jimbo la Haut-Katanga.

Wanachama hao wa UDPS walikamatwa jana Jumapili wakati wakihudhuria mkutano kwenye makao makuu ya chama hicho, ambapo magari matatu ya jeshi la polisi nchini humo yalizingira eneo hilo na kuwezesha wanajeshi wa serikali kuingia kwenye mkutano na kuwatia nguvuni  wanachama hao.

Mkuu wa MONUSCO, Maman Sidikou amesihi mamlaka za DRC kuwaachia huru bila masharti  na pia kuheshimu uhuru wa msingi na haki za kiraia na kisiasa za watu wote.

MONUSCO inasisitiza pia  kwachiwa huru kwa Bwana Kyungu wa Kamwanza, rais wa kitaifa wa Chama cha upinzani cha UNAFEC, ambaye amefungwa kwa muda wa miezi kadhaa.

Photo Credit
Mkuu wa MONUSCO, Maman Sidikou.(Picha:UM/Kim Haughton)