Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UM nchini CAR azungumza na wagombea urais

Mkuu wa UM nchini CAR azungumza na wagombea urais

Pakua

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR Parfait Onanga-Anyanga amekutana leo na wagombea urais 28 miongoni mwa 30 waliogombea katika uchaguzi uliofanyika tarehe 30, Disemba, mwaka 2015.

Taarifa hizo ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric aliyezungumza na waandishi wa habari leo mjini New York Marekani akisema kwamba bwana Onanga-Anyanga amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mchakato wa uchaguzi.

Ameongeza kwamba wagombea hao wa urais wameahidi kuwasilisha kwenye Mahakama ya Kikatiba malalamiko yao yanayohusiana na uchaguzi kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi.

Aidha Bwana Dujarric amesema asilimia 98 ya matokeo ya uchaguzi ya rais na asilimia 96 ya matokeo ya uchaguzi wa wabunge yamepokelewa na kituo cha takwimu kwenye mji mkuu Bangui.

Matokeo ya kura za wakimbizi waliopo nchini Cameroon, Chad, Jamhuri ya Congo na Sudan nayo pia yameshawasilishwa.

Photo Credit
Parfait ONanga-Anyanga akizungumza na wagombea urais wa CAR. Picha ya MINUSCA.