Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MUHTASARI: WFP Gaza, Sikua ya Nelson Mandela na Ukiukwahi wa haki rumande CAR

Chakula cha moto kinagawiwa na WFP Gaza
© WFP/Mostafa Ghroz
Chakula cha moto kinagawiwa na WFP Gaza

MUHTASARI: WFP Gaza, Sikua ya Nelson Mandela na Ukiukwahi wa haki rumande CAR

Amani na Usalama

Katika Muhtasari  wa habari hii leo tunaangazia changamoto ya WFP katika kusambaza chakula Gaza, leo pia ni siku ya  kimataifa ya Nelson Mandela na  nchini Jamhuri ya Kati CAR ripoti  ya Umoja wa  Mataifa inasema kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu rumande

Katika Ukanda wa Gaza leo shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP limeonya kwamba amri ya hivi karibuni kabisa ya Jeshi la Israel ya watu kuondoka Gaza imesababisha idadi kubwa zaidi ya watu kutawanywa tangu mwezi Oktoba mwaka jana.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao  wa kijamii wa X shirika hilo limesema  vituo vingi vya ugawaji wa chakula vimefungwa na maduka machache tu ya kuoka mikate ndio yanafanya kazi hivyo limesema “Tunahitaji haraka ongezeko la usambazaji wa chakula na uwezo mkubwa wa kuweza kugawa chakula cha moto kilicho tayari kuliwa ili kuokoa maisha.”

Mkutano usio rasmi wa Baraza Kuu katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Nelson  Mandela
UN Photo/Loey Felipe
Mkutano usio rasmi wa Baraza Kuu katika kuadhimisha siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela

Leo ni siku ya kimtaifa ya Nelson Mandel mwaka huu ikibeba maudhui “Bado ni jukumu letu kutokomeza njaa na pengo la usawa” Katika ujumbe wake wa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, Nelson Mandela alituonyesha tofauti kubwa ambayo inaweza kuletwa na mtu mmoja katika kujenga Ulimwengu bora hivyo” Tunaweza kuchagua kutokomeza umasikini, tunaweza kuchagua kutokomeza pengo la usawa. Tunaweza kuchagua kufanyaia mabadiliko uchumi  wa kimataifa na mifumo ya fedha kwa jina na usawa na tunaweza kuchagua kupambana na ubaguzi wa rangi, kuheshimu haki za binadamu, kupambana na mabadiliko ya tabianchi na  kujenga dunia  ambayo inafaa kwa binadamu wote. Kila mmoja wetu anaweza kuchangia kupitia hatua kubwa na ndogo.”

Wafungwa katika jela ya wanawake ya  Bimbo nchini CAR wakiadhimisha siku ya Nelson Mandela
MINUSCA / Leonel GROTHE
Wafungwa katika jela ya wanawake ya Bimbo nchini CAR wakiadhimisha siku ya Nelson Mandela

Hatua za haraka na madhubuti zinahitajika ili kuhakikisha kuheshimiwa kwa haki za binadamu katika vituo vya rumande nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, ambako mateso na unyanyasaji, kukamatwa na kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria na kiholela, utapiamlo na huduma duni za afya vimetawala, kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati MINUSCA.

Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk amesema "Matokeo ya ripoti hii yanatia wasiwasi na yanahitaji hatua za haraka na madhubuti kutoka kwa mamlaka ya kitaifa. Mageuzi yanayoendelea katika mfumo wa jela yanatoa fursa muhimu kwa CAR kushughulikia ukiukwaji huu mkubwa wa haki za binadamu.”