Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pumba za mchele zatumika kutengeneza mkaa safi na salama

Pumba za mchele zatumika kutengeneza mkaa safi na salama
UNIDO/ITPO Tokyo
Pumba za mchele zatumika kutengeneza mkaa safi na salama

Pumba za mchele zatumika kutengeneza mkaa safi na salama

Tabianchi na mazingira

Nchini Japani, teknolojia ya kutengeneza mkaa kwa kutumia pumba za mpunga badala ya mkaa imepata umaarufu na kusambazwa nchi za Afriak na Asia na hii ni kutokana na kazi za shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO.

Kupitia ofisi yake ya kuendeleza Uwekezaji na Teknolojia, ITPO nchini Japan, shirika hilo limeweza kukutanisha kampuni iliyobuni teknolojia na kampuni kubwa na hivyo kuepusha matumizi ya nishati ya kupikia inayotumia miti na badala yake kutumia pumba za mpunga. 

Fumio Adachi, ITPO Tokyo akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Manama, Bahrain hivi karibuni ametaja kampuni hiyo ndogo ya kijapani kuwa ni Tromso. 

Amesema kampuni hiyo ni ndogo sana lakini eneo hilo ni mashuhuri kwa teknolojia zinazohusiana na ujenzi wa meli. Teknolojia hiyo ya kujenga meli ni ya juu sana. Kwa hiyo kampuni imetumia teknolojia hiyo kuunda mashine maalum au kinu cha kugandamiza pumba za mpunga.” 

Fumio Adachi, Mkuu wa UNIDO/ITPO Tokyo
UN Video
Fumio Adachi, Mkuu wa UNIDO/ITPO Tokyo

Pumba hizo hugandamizwa na mashine hiyo na kinachopatikana kinaweza kutumika kwa ajili ya kupikia au chanzo cha nishati. 

Kwa mujibu wa Bi. Adachi, kampuni nyingi zina teknolojia hiyo, lakini hii ya Tromso inagandamiza pumba za mchele kwa kiwango cha juu na hatimaye kukatwa vipande vipande kama vya mkaa au BRIKETI na wakati vinasafirishwa haviwezi kusambaratika. 

Tromso ilibisha hodi ITPO Japani

Hii kampuni ilifika ofisini kwetu kwa sababu kila wakati tunasema tunaweza kupatia  nchi zinazoendelea taarifa kuhusu teknolojia zinazobuniwa na kampuni za kijapani. Kwa hiyo kampuni hii ilifika na kutuonesha  teknolojia yao na mara moja tulibaini kuwa inaweza kutumika kwenye nchi zinazoendelea. 

UNIDO inasema kuwa mantiki ya teknolojia hii ni suala kwamba kila mwaka mamilioni ya ekari za misitu hukatwa kwa ajili ya kuni au mkaa wa kupikia majumbani, ambazo moshi wake husababisha madhara ya kiafya, kwa mujibu wa ripoti mpya ya Haliya Hewa duniani, SoGa iliyotolewa hivi karibuni na UNICEF kwa ushirikiano na taasisi ya Health Effects au HEI. 

Ukataji miti kwa ajili ya nishati pia husababisha kuenea kwa jangwa. Na wakati huo huo, mpunga katika nchi zinazoendelea baada ya kukobolewa, pumba zinazobakia hazitumiki ipasavyo. 

Mchakato wa kutengeneza mkaa kutoka kwenye pumba 

Sasa mashine iliyotengenezwa na TROMSO inasagisha pumba na kuzikandamiza hadi zinakuwa ngumu na kisha zinapitishwa kwenye kiwango cha juu cha joto. Baada ya hapo hukatwa vipande vipande vya kuweza kutumika kama mkaa au BRIKETI. 

Pumba za mpunga.
UNIDO/ITPO Tokyo
Pumba za mpunga.

Bi. Adachi anasema, “tulialika mabalozi mjini Tokyo, na baadhi ya mabalozi walibaini mara moja walielewa kuwa wanataka kupeleka teknolojia hiyo kwenye nchi zao, hasa nchi za Afrika. Hivyo basi, kampuni hii ndogo yenye wafanyakazi 10 na iliyoko mji wa Hiroshima ulioko mbali na Tokyo, iliweza kupeleka teknolojia yake kwa nchi nyingi za Afrika. 

Ushindi kwa pande zote 

Sasa kampuni kubwa za biashara za Japan zina uhusiano na kampuni hii ndogo ya Japani, na hii kampuni ndogo sasa ina uhusiano mzuri na nchi nyingi zinazoendelea. Na huu ni Ushindi kwa pande zote kwa kampuni hii ndogo ya Japan na vile vile kwa nchi zinazoendelea. 

Je mkaa wa pumba za mpunga una madhara? 

Tathmini ilifanyika kubaini iwapo moshi na hewa kutoka kwenye mkaa uliotengenezwa kwa pumba za mchele una madhara ya kiafya au la, na ilidhihirika kuwa hakuna viashiria vyovyote vya hewa chafuzi kama vile Naitrojeni Daioksaidi. 

Tangu mwaka 2007 zaidi ya vinu 90 vya kusagisha pumba za mchele zimenunuliwa Japani na kupelekwa Nigeria, Tanzania, Vietnam na China. Kwa TROMSO teknolojia hii itafaa sana kwenye maeneo ya wakimbizi ambako miti hukatwa kwa ajili ya kuni, na zaidi ya yote Afrika kwani malighafi ambazo ni pumba za mahindi zinapatikana.