Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hataza kwenye tafiti kukwamua kiuchumi wahadhiri Vyuo Vikuu

ya Mhandisi Dokta Adesuwa Queeneth Kingsley-Omoyibo,  Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Igbinedion kilichoko mji wa Okada jimboni Edo nchini Nigeria
UN News/Assumpta Massoi
ya Mhandisi Dokta Adesuwa Queeneth Kingsley-Omoyibo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Igbinedion kilichoko mji wa Okada jimboni Edo nchini Nigeria

Hataza kwenye tafiti kukwamua kiuchumi wahadhiri Vyuo Vikuu

Ukuaji wa Kiuchumi

Tafiti zinazofanywa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu duniani kote zisisalie kwenye makabrasha na makabati bali zifanyiwe mchakato wa miliki ya ubunifu na hatimaye zigeuke chanzo cha kipato kwa wahadhiri hao, jambo litakalofanikisha harakati za kuondokana na umaskini.

Ni kauli ya Mhandisi Dokta Adesuwa Queeneth Kingsley-Omoyibo,  kutoka Chuo Kikuu cha Igbinedion kilichoko mji wa Okada jimboni Edo nchini Nigeria alipohojiwa na Idhaa yaUmoja wa Mataifa wakati wa jukwaa la 4 la Uwekezaji kwa Wajasiriamali, WEIF2024 lililokunja jamvi wiki mbili zilizopita huko Manama, Bahrain.

Jukwaa hilo lililenga kuchagiza ujasiriamali na  ubunifu kwa ajili ya kusongesha malengo ya maendeleo endelevu. Liliandaliwa na wadau mbali mbali likiwemo shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO, ofisi yake ya kuendeleza Ubunifu na Teknolojia, ITPO nchini Bahrain.

Zaidi ya wajasiriamali 1000 wakiwemo wanamuziki, wabunifu wa mitindo, wanazuoni kutoka nchi 84 walishiriki na Mhandisi Dokta Kingsley-Omoyibo akasema kilichomleta yeye kwenye jukwaa hilo ni kufuatilia usimamizi wa miliki ya ubunifu hasa kwa tafiti zinazofanywa na wahadhiri wa Vyuo Vikuu.

Anasema “wahadhiri wa Vyuo Vikuu wako hapa ambao wanafanya tafiti na baada ya kuandika machapisho, vyote huishia kwenye makabati. Hapana! Hapana! Lazima igeuzwe iwe biashara.  Kwa hiyo kila tafiti itakapogeuzwa kuwa biashara, italeta fedha, itainua nafasi ya Chuo Kikuu kwenye orodha ya vyuo kwa kwani machapicho yanaweza pia kuwa mtandaoni na pia kwenye majarida ya ngazi ya juu.”

Mhandishi Dokta Kingsley-Omoyibo anaongoza kitengo cha Miliki ya Ubunifu na Usongeshaji wa Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Igbinedion nikamuuliza jukumu hasa la kitengo hicho na akasema kila mwaka wanazungumza na wahadhiri wakiwahoji kuhusu tafiti na machapisho yao.

Wanachoulizwa wahadhiri baada ya kuchapisha tafiti

Hebu tuone umefanya nini? Una ugunduzi au una ubunifu, basi leta tuiwekee hataza. Tunakufundisha jinsi ya kutafuta mtandaoni, tunaita kusaka hataza. Na kama kuna mtu amefanya ulichofanya, tunachambua tuone kama una kitu kipya zaidi kwenye utafiti wako. Basi tukiona una kitu kipya, unapaswa kuwekea hataza. Haki ya hataza inadumu kwa miaka 20.  Na kwa kipindi hicho unapatiwa leseni ya kumiliki ugunduzi na ubunifu huo.

Hataza ambayo ni miongoni mwa miliki za ubunifu, kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili ni waraka wa kisheria unaotolewa kwa mgunduzi wa kitu unaokataza watu wengine kuiga ubunifu huo.

Nini faida ya wahadhiri kuwa na hataza?

Unapomiliki unakuwa umeiwekea hataza. Kwa hiyo unavyokuwa na hataza nyingi , mosi, unatambulika na Chuo Kikuu; Pili unajipatia fedha; na tatu unahamisha watu wengine nao kuwa na hataza zao.

Ili Kuhamasisha jamii ya wanazuoni kuelewa kuhusu miliki ya ubunifu Mhandisi Dokta Kingsley amesema huendesha warsha kuelimisha kuhusu hataza, haki za kunakili pamoja na alama za biashara na wanachotaka ni kuona wahadhiri wabunifu na wagunduzi wanakuwa wajasiriamali wa teknolojia au Technopreneur. 

Hataza na ujasiriamali Vyuo Vikuu

Na pindi wahadhiri wa Vyuo Vikuu wakiamua kufanya hivi, dunia itakuwa pahala bora. Kwa sababu tunahitaji  kuhamasisha wanafunzi wetu wawe na fikra za kijasiriamali na ndio maana tumeanzisha fikra za ujasiriamali kwa wanafunzi wetu ili waimarike kijasiriamali, waajirike, waingie kwenye soko la ajira,  badala ya kukaa nyumbani bila kufanya chochote. Na wawe chachu kwenye dunia na kisha dunia iwe pahala bora.

Ubunifu mwelekeo mpya wa kuinuka kiuchumi

Katika jukwaa la WEIF suala la uchumi utokanao na kazi za ubunifu au Orange Economy, lilipatiwa kipaumbele na hapa akiwa amezingirwa na kazi za sanaa kama vile uchoraji nikamuuliza nini umuhimu wa wasanii kusajili kazi zao?

Hakusita kujibu akisema, “miliki ya ubunifu ni muhimu sana. Je ni nini ? Ni wazo lako, ni kile unachomiliki hivyo hakuna mtu yeyote anatakiwa kukunyang’anya. Kama mtu amechora kazi hii ya sanaa, hakuna mtu yeyote anapaswa kuinakili. Sasa tunafanya nini? Hii inapaswa kusajiliwa hataza  ili mtu asiibe au kunakili. Na iwapo mtu atanakili, basi mtu huyo amefanya uhalifu wa wizi wa miliki ya ubunifu na anaweza kwenda jela.”

Wito wake kwa wajasiriamali wa ubunifu ni “hebu tuwahamasishe wajasiriamali wetu wasajili hataza za kazi zao ili watu wasiwanyemelee na kuiba miliki zao za ubunifu.”