Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Harakati za uwekezaji kwa wajasiriamali duniani kumulikwa Manama, Bahrain

Dkt. Hashim Hussein, Mtaalamu wa kuendeleza uwekezaji katika shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO akizungumza na Assumpta Massoi huko Bahrain.
UN News/Abdelmonem Makki
Dkt. Hashim Hussein, Mtaalamu wa kuendeleza uwekezaji katika shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO akizungumza na Assumpta Massoi huko Bahrain.

Harakati za uwekezaji kwa wajasiriamali duniani kumulikwa Manama, Bahrain

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Jukwaa la 5 la kimataifa la uwekezaji kwa wajasiriamali, WEIF 2024 linaanza kesho kwenye mji mkuu wa Bahrain, Manama ukileta pamoja washiriki zaidi ya 1000, wakiwemo wajasiriamali kutoka pembe zote za dunia. Jukwaa hili linafanyika kwa siku tatu na na maudhui ni kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kwa kuendeleza uvumbuzi na ukuaji wa kiuchumi. Jukwaa hili linalenga basi kupatia majawabu changamoto za dunia ikiwemo umaskini, ukosefu wa usawa, mabadiliko ya tabianchi, amani, haki kwa muktadha wa SDGs.

Tweet URL

Pilikapilika za maandalizi zinaendelea kwani kutakuweko na mikutano ya ndani na vile vile maonesho. Katika mikutano kutakuwa majopo ya wataalamu wakimulika masuala kama vile kujenga ubia endelevu kwa lengo la kuunda mustakabali bora kwa wajasiriamali kutoka nchi za kiarabu na zile za kiafrika. Katika jopo hili, Bi. Olive Zaitun Kigongo, Rais wa Chama cha wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka Uganda atazungumza.

Ni mikutano na maonesho

Kuna mjadala pia kuhusu ujumuisha kifedha endelevu na umuhimu wa sekta ya ujasiriamali utokanao na ubunifu iwe kwenye Sanaa kama vile muziki na kazi za mikono, halikadhalika wanawake wajasiriamali kwenye maeneo baada ya mizozo.

Kando ya mikutano kutakuwa na maonesho makuu manne. Mosi ni kundi la watu wenye ulemavu na ugunduzi, pili; Familia zilizo fanisi, tatu: uchumi usioharibu mazingira na nne, uchumi utokanao na kazi bunifu kwenye sanaa kwa lugha ya kiingereza ikiitwa Orange economy.

Azimio la Tano la Manama

Nimezungumza na Dkt. Hashim Hussein, yeye ni mtaalamu wa kuendeleza uwekezaji katika shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO hapa Bahrain ni nini hasa wanatarajia kutoka jukwaa hili?

“Kila mara tunakuwa na azimio ambapo tutakuwa na Azimio la Manama namba 5 la mwaka 2024 na tutaliwasilisha kwenye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa New York hasa wakati huu kuna mkutano wa zama zijazo utakaofanyika New York, mwezi Septemba. Tunajikita kimataifa lakini nchi za kiarabu na Afrika kwani zinahitaji  usaidizi zaidi. Hivyo tutaangalia ni vipi tutaliwasilisha kwenye mkutano wa zama zijazo. Bila shaka kutakuwa na maombi lukuki kwani wajasiriamali wana mahitaji mengi na kadri wanavyohitaji vivyo  hivyo tunawasilisha kwa jamii ya kimataifa.”

Wajasiriamali wanawake kutoka nchi zenye mizozo watakuweko

Nilimuuliza kuhusu mjadala kuhusu wanawake wajasiriamali kwenye maeneo baada ya mizozo na akasema.

“ Tutakuwa na mifano kutoka Afghanistan, Palestin hususan Gaza na Sudan. Halikadhalika nchi za Ukanda wa Sahel ambazo ni Burkina Faso, Mali, Chad na Niger na Mauritania. Nchi hizo zina mizozo iliyodumu muda mrefu ndani ya nchi zao lakini kuna pia tatizo la uhamiaji. Kuna changamoto nyingi sana. Iwapo utawapatia stadi sahihi,  hawatokimbia nchi zao. Tunataka kujikita kwa wanawake kwa kuwa wao ndio wanapata shida zaidi baada ya mizozo, wanakuwa wajane, wanalea familia peke yao. Hivyo wanahitaji kipato. Tunataka kujadili na tupate mbinu ya jinsi gani ya kusaidia wanawake baada ya mizozo.”

Dkt. Hashim Hussein, Mtaalamu wa kuendeleza uwekezaji katika shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO akizungumza na Assumpta Massoi huko Bahrain.
UN/Hisae Kawamori
Dkt. Hashim Hussein, Mtaalamu wa kuendeleza uwekezaji katika shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO akizungumza na Assumpta Massoi huko Bahrain.

Ugunduzi unaweza kufanikisha SDGs

UNIDO inasema ugunduzi unaweza kufanikisha kuendelezwa kwa teknolojia mpya, bidhaa na huduma ambazo zinaweza kuwa majawabu ya changamoto za kijamii na kimazingira.  Jukwaa hili linatambua kuwa ugunduzi na ukuaji wa kiuchumi ni viwezeshi muhimu katika kufanikisha SDGs.

Hivyo basi ni vema kuendeleza ujasiriamali, kuhamasisha ujasiriamali, kuwekeza kwenye tafiti na maendeleo, kujenga utamaduni wa ugunduzi na ubunifu kwa kuthamini ubunifu.

Jukwaa hili limeandaliwa kwa ufadhili wa Mwanamfalme wa Bahrain Salman Bin Hamad Al Khalifa ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Bahrain huku likiratibiwa na sekretarieti ya Ofisi ya UNIDO ya kusongesha Uwekezaji na Teknolojia Bahrain, ITPO kwa ubi ana Umoja wa nchi za kiarabu, serikali ya Bahrain, Umoja wa vyama vya kibiashara urabuni, Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya kiuchumi kwa Afrika, Chama cha Biashara Bahrain na wadau wengine wengi wa kikanda na kimataifa.