Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Heshimu nguvu na ujasiri wa wakimbizi

Mkimbizi wa Congo ambaye ni mfanyakazi wa uchomeleaji kutoka kambi ya Kakuma nchini Kenya.
© UNHCR/Charity Nzomo
Mkimbizi wa Congo ambaye ni mfanyakazi wa uchomeleaji kutoka kambi ya Kakuma nchini Kenya.

Heshimu nguvu na ujasiri wa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Wakimbizi, Umoja wa Mataifa umeitumia siku hii kutoa wito wa mshikamano na wakimbizi kote duniani.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anasema, "wanapopewa fursa, wakimbizi hutoa mchango mkubwa kwa jamii zinazowahifadhi. Wanahitaji kupata fursa sawa na kazi, makazi na huduma za afya. Wakimbizi wenye umri mdogo wanahitaji elimu bora ili kufikia ndoto zao."

"Migogoro, mabadiliko ya tabianchi na machafuko" yamewalazimu zaidi ya watu milioni 120 kutoka kwa makazi yao wakiwemo milioni 43.5 ambao wamekimbia kuvuka mipaka ya kitaifa amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake mahususi kwa ajili ya siku hii muhimu kwa wakimbizi.

"Hebu tuahidi kuthibitisha jukumu la pamoja la ulimwengu katika kusaidia na kukaribisha wakimbizi", kutetea haki zao za kibinadamu - ikiwa ni pamoja na kupata hifadhi  na hatimaye, kusaidia kutatua migogoro ambayo inang'oa wengi.” Amesisitiza.

Miaka miwili baada ya jukwaa la kimataifa kuhusu wakimbizi, Rwanda imeonesha kwa vitendo sera yake ya ujumuishi wa wakimbizi na wenyeji wao
UN Video
Miaka miwili baada ya jukwaa la kimataifa kuhusu wakimbizi, Rwanda imeonesha kwa vitendo sera yake ya ujumuishi wa wakimbizi na wenyeji wao

Filippo Grandi

Naye Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR) Filippo Grandi amesisitiza kuwa suala la kuwajumuisha wakimbizi linapaswa kuwa la kawaida akiongeza kwamba wakimbizi wanaofika mipakani sio tu suala la nchi tajiri, na ukweli ni kuwa “robo tatu ya wakimbizi duniani wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini au cha kawaida na ni uongo, na kutowajibika kudai kwamba wengi wanajaribu kwenda Ulaya au Marekani."

Bwana Grandi amewaenzi mamilioni ya watu kote ulimwenguni ambao wanalazimika kukimbia kutokana na migogoro na mateso.  Aidha amewapongeza  wakimbizi kwa ustahimilivu wao na uwezo wao wa kuanza upya, licha ya changamoto za kutisha wanazokabiliana nazo.

Kuhusu Sudan Kusini

Akizungungumza kutoka Jamjang, Sudan Kusini, Grandi amesema kuwa hali ya ukimbizi katika nchi hiyo  ni ya kutisha mno. Amesema kuwa “katika miezi ya hivi karibuni, karibu watu 700,000 wamevuka kutoka Sudan jirani, wakikimbia vita vikali ambavyo vimewaondolea makazi yao, wapendwa wao kila kitu.” 

Mfanyakazi wa misaada ya kibinadamu akichunguza utapiamlo kwenye kambi kwa watu waliokimbia makazi yao huko Malakal, Sudan Kusini
© UNOCHA/Sarah Waiswa
Mfanyakazi wa misaada ya kibinadamu akichunguza utapiamlo kwenye kambi kwa watu waliokimbia makazi yao huko Malakal, Sudan Kusini

Grandi ameeleza kuwa ingawa awali baadhi ya  watu walikimbia nchi hii ili kuepuka vita vya wenyewe kwa wenyewe, sasa wanalazimishwa kurudi mahali ambapo bado panapambana kupona kutokana na miaka ya mapigano na njaa. Amesema “Wengine ni Wasudani – walimu, madaktari, wafanyabiashara na wakulima ambao sasa wanapaswa kukabiliana na maisha kama wakimbizi.

Wakimbizi wanaofika mipakani sio suala tu kwa nchi tajiri kwani robo tatu ya wakimbizi duniani wanaishi katika nchi zenye mapato ya chini au ya wastani . “Ni uongo na siyo haki kudai kwamba wengi wanajaribu kwenda Ulaya au Marekani.” Ameeleza.

Kuhusu janga linaloendelea Sudan, Grandi ametaja Sudan Kusini, Chad, Ethiopia na Misri kama nchi ambazo zinatoa hifadhi kwa watu wa Sudan wanaokimbia hofu.

Watoto na familia zao wanasimama karibu na makazi ya muda katika kambi ya IDPs katika mji wa Zelingei, Darfur ya kati, Sudan.
© UNICEF/Antony Spalton
Watoto na familia zao wanasimama karibu na makazi ya muda katika kambi ya IDPs katika mji wa Zelingei, Darfur ya kati, Sudan.

Ingawa nchi hizi zinaonesha kwamba mshikamano unawezekana hata katika chini zenye mazingira magumu zaidi, Grandi anaonya kuwa hawawezi kufanya hivyo peke yao. Amesema “katika wakati wa mgawanyiko na msukosuko, wakimbizi  na wale wanaowahifadhi  wanahitaji sisi sote tushirikiane.”

Kamshina huyu anaonya kuwa migogoro inaendelea kuongezeka duniani lakini uwezo wa kisiasa wa kutatua migogoro hiyo unaonekana kutokuwepo. “Na hata wakati migogoro hii ikiongezeka, haki ya kutafuta hifadhi iko hatarini. Na kufanya hali kuwa mbaya zaidi, athari za kimataifa za mabadiliko ya hali ya tabianchi zinaongezeka ,ikiwemo, mafuriko makubwa yanayotarajiwa kuzamisha vijiji na mashamba, na kuongeza kwa kiwango kikubwa changamoto zinazokimba Sudan Kusini.” Ameongeza.

Mpango mpya wa maendeleo nchini Kenya utabadilisha kambi za wakimbizi za zamani kuwa makazi ambapo wakimbizi watapata fursa zaidi za kuendelea, na upatikanaji kamili wa huduma mbalimbali.

Lengo la mustakabali ni  hatua endelevu katika elimu, nishati, usalama wa chakula, ajira, makazi na zaidi,  kwa kushirikiana na serikali, washirika wa maendeleo na wengineo. Grandi pia ametoa wito wa kutowaacha wakimbizi kati hali ya sintofahamu na badala yake, kuwapa nafasi ya kutumia ujuzi na vipaji vyao na kuchangia kwenye jamii zilizowakaribisha.

Muhidin Libah alianzisha Jumuiya ya Watu wa Kisomali huko Lewiston Maine marekani, ambapo Wakimbizi wa zamani 220 kutoka Somalia ambao walikaa miaka mingi katika kambi zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Kenya wamepanda mbegu ya maisha mapya kat…
UN News/Daniel Dickinson
Muhidin Libah alianzisha Jumuiya ya Watu wa Kisomali huko Lewiston Maine marekani, ambapo Wakimbizi wa zamani 220 kutoka Somalia ambao walikaa miaka mingi katika kambi zinazoungwa mkono na Umoja wa Mataifa nchini Kenya wamepanda mbegu ya maisha mapya katika jimbo la Maine nchini humo.

Njia salama

Grandi ameongeza kuwa  “ lazima kuwe na njia salama na za kisheria za wakimbizi kuhamia sehemu nyingine, iwe kupitia viza za kazi, udhamini wa masomo au makazi mapya katika nchi nyingine.” Ameonya kwamba  bila chaguzi hizi, watu wengi zaidi watageuka kuwa wafanyabiashara haramu katika harakati za kutafuta matumaini na fursa.

Ametamatiza kwa  kuomba ufadhili wa kimataifa ili kusaidia wale wanaokimbia vita Sudan, na kuwezesha mamlaka za ndani na jamii zinazowahifadhi kupanua miundombinu, makazi na huduma. “sote tunaweza kufanya zaidi kuonyesha mshikamano na wakimbizi na kufanya kazi kuelekea dunia ambapo wanakaribishwa, au wanaweza kurudi nyumbani kwa amani. Kwa ujasiri, kujitolea na huruma, suluhisho ziko ndani ya uwezo wetu.” Amesema.