Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilikuwa mwathirika wa ajira ya watoto lakini sasa nafanya kila niwezalo kuizuia: Daniel Berruezo

Daniel Berruezo mfanyakazi wa wizara ya kazi ya Argentina jimboni Salta
© ILO/Gastón Chedufau
Daniel Berruezo mfanyakazi wa wizara ya kazi ya Argentina jimboni Salta

Nilikuwa mwathirika wa ajira ya watoto lakini sasa nafanya kila niwezalo kuizuia: Daniel Berruezo

Haki za binadamu

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga ajira kwa watoto ambayo mwaka huu imebeba maudhui “Hebu tutekeleze ahadi zetu kukomesha ajira ya watoto” tunaelekea nchini Argentina kukutana na muathirika wa ajira ya watoto ambaye sasa  ameamua kulivalia njuga suala hilo na anafanya juu chini kuitokomeza ajira kwa watoto ambayo imekita mizizi nchini humo kwa miaka nenda miaka rudi.  

Kwa mujibu wa shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO ajira kwa watoto ni ukiukwaji mkubwa wa haki zao n ani uhalifu unaokwenda kinyume na sheria na mikataba ya kimataifa ya kazi lakini pia ni kosa la jinai.

Jimboni Salta nchini Argentina kutana na Daniel Berruezo mfanyakazi wa serikali katika wizara ya kazi jimboni Salta akifanya kazi ya kutokomeza ajira kwa watoto ambayo nchini humo imekita mizizi . Daniel anasema“Ajira kwa watoto imekuwa ni jambo la kawaida na watu wanadhani hiyo ni sawa na ni haki kwa watoto kufanyakazi.”

Kaka yangu pamoja nami wakati tulipoanza kufanya kazi kwenye mashamba ya tumbaku
© Daniel Berruezo
Kaka yangu pamoja nami wakati tulipoanza kufanya kazi kwenye mashamba ya tumbaku

Wahenga walinena asifiaye mvua imemnyea ndivyo ilivyokuwa kwa Daniel katika utoto wake “Katika kisa changu nilikuwa na miaka 7 tu na kaka yangu mika 8, tulianza ajira kama wafanyakazi wa tumbaku kila mwaka kuanzia Desemba hadi mwezi Machi tulipokuwa katika likizo za shule, tulilima Katia mashamba ya tumbaku, ujira tuliokuwa tukilipwa tulinunua vifaa vya shule na nguo kwa ajili ya mwaka mzima wa masomo.”

Daniel Berruezo alifanyakazi katika moja ya mashamba haya ya tumbaku
© ILO/Gastón Chedufau
Daniel Berruezo alifanyakazi katika moja ya mashamba haya ya tumbaku

Mapambano dhidi ya ajira kwa watoto

Alipofikisha umri wa miaka 22 Daniel aliacha kuajiriwa na akashika usukani wa kusimamia shamba la tumbaku na kuliendesha hadi alipofikisha umri wa miaka 28 alipoamua kujiunga na wizara ya kazi katika jimbo la Salta anasema “Wakati huo tuliona haja ya kupeleka timu kutoka wizara ya kazi kwenda kwenye bonde la eneo la Lerma ili tuweze kufuatilia sio tu kazi ambazo hazijatanabaishwa lakini pia ajira kwa watoto. Kwa sababu ya uzoefu wangu nilikuwa na kila kigezo kwa jukumu hilo. Nilikuwa kwenye ajira ya watoto, mfanyakazi wa tumbaku na mzalishaji wa tumbaku.”

Kupitia kazi yake Daniel alipata kozi maalum ya kuzuia ajira kwa watoto “Tulijifunza jinsi ya kubaini ajira kwa watoto, jinsi ya kutekeleza será zinazohusu ajira kwa watoto na kuhusu kuwalinda vijana barubaru wanaofanyakazi.”

Naelewa jinsi ilivyo kufanyakazi kwenye mashamba ya tumbaku. Hapo ni mimi nilipokuwa kijana barubaru
© Daniel Berruezo

Kwa Daniel ni muhimu sana kile alichokipitia kisijirudie kwa watoto wake na anatamani siku moja hii iwe hali halisi kwa watoto wake kutoajiriwa utotoni  “Nia watoto wawili msichana na mvulana. Nadhani kitu cha kwanza unachofanya ni kuwalinda wasifanye kazi. Wafundishe vitu na thamani ya vitu, lakini daima epuka kuwaacha wafanye kazi tangu wakiwa watoto. Ndoto yangu ni kutokomezwa kwa ajira ya watoto na nafikiri hiyo ni ndoto ya watu wengi kwamba kusiwe na watoto wanaofanyakazi. Hatua zimepigwa na niña furahia sana kuhusu hilo lakini bado tuna kibarua zaidi cha kufanya.”