Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kwa nini kuboresha usalama wa chakula ni muhimu?

Mkono wa muuzaji hufikia kwenye kibanda cha soko kinachoonyesha nyanya, karoti, na kolantro.
© WHO/Quinn Mattingly Mboga yakiuzwa katika soko dogo la ndani katika kijiji cha Doi Son, Mkoa wa Ha Nam, Vietnam.

Kwa nini kuboresha usalama wa chakula ni muhimu?

Afya

Kila tarehe 7 Juni, dunia inaadhimisha Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula, siku inayoangazia matukio mbalimbali ya usalama wa chakula katika pande zote za ulimwengu. Kwa mwaka huu 2024, maadhimisho hayo yamekuja na kaulimbiu inayosisitiza umuhimu wa kuwa tayari kwa matukio ya usalama wa chakula.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) linasema tani milioni 931 sawa na asilimia 17 ya chakula kilichozalishwa, kiliishia kwenye mapipa ya taka ya kaya, wauzaji, migahawa na wadau wengine wa chakula.”

Wakati huo huo, watu milioni 811 wana njaa na milioni 132 leo hii wanakabiliwa na kutokuwa na uhakika wa chakula na lishe bora.

Shirika hilo limeongeza kuwa chakula kisichotumiwa hupoteza rasilimali kama vile ardhi, maji, nishati, udongo, mbegu na pembejeo zingine zinazotumika kwa uzalishaji wake.

Kwa mujibu wa mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula (INFOSAN), inaeleza usalama wa chakula ni pamoja na kutafuta njia sahihi za kuhifadhi na kufanya upya uzalishaji wa chakula kilichoisha matumizi, na hii inaweza kutupilia mbali tatizo la njaa duniani.

Wanawake wawili waliovalia vyandarua vya nywele na makoti ya maabara wakiweka lebo kwenye mitungi ya chakula katika kiwanda huko Manzini, Eswatini.
© FAO/Giulio Napolitano FAO imezindua mfumo wenye zana za kusaidia wale wote wanaofanya kazi katika sekta ya chakula kuzingatia viwango vya kimataifa vya usafi wa chakula. (Maktaba)

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni  (WHO) linafafanua matukio ya usalama wa chakula kuwa ni hali ambapo hatari ya afya inayotokana na matumizi ya chakula inapothibitishwa, ingawa kuwa tayari kudhibiti matukio ya usalama wa chakula kunahitaji juhudi za kujitolea kutoka kwa watunga sera, mamlaka ya usalama wa chakula, wakulima na waendeshaji biashara ya chakula na watumiaji pia wanaweza kuchukua jukumu kubwa.

Katika kuthibitisha ukubwa wa tatizo la usalama wa chakula, WHO inaeleza kuwa kila mtu mmoja kati ya watu 10 anaugua kutokana na kula chakula ambacho si salama, na takribani watu 420,000 duniani kote hufa kila mwaka baada ya kula chakula kilichochafuliwa na watoto chini ya umri wa miaka 5 hubeba asilimia 40 ya mzigo wa magonjwa ya chakula, na vifo 125,000 kila mwaka.

Mwaka 2004, FAO kwa kushirikiana na WHO ziliunda Mtandao wa Mamlaka ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula (INFOSAN) kama wadau wakati wa matukio ya usalama wa chakula na uripoti dharura za kimataifa ili kufanya hesabu ya matukio ya usalama wa chakula  kila mwaka na kufanya tathmini ya jinsi gani ya kuepukana na matukio hayo ya usalama wa chakula duniani. 

Mtazamo wa karibu wa matunda mapya, ikiwa ni pamoja na pichi, tufaha, na matikiti maji, kwenye kreti sokoni nchini Italia. Wanunuzi na muuzaji wanaonekana kwenye mandharinyuma yenye ukungu.
FAO/Alessandra Benedetti Soko katika chama cha ushirika cha chakula katika shamba la ushirika la Orto Sole huko Fiumicino na Torrimpietra, Italia. Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) limetoa wito wa kuwepo kwa lishe bora zaidi ya afya na uwiano katika Ulaya na Asia ya Kati.

Je, wajua?

*Chakula kisicho salama chenye bakteria hatari, virusi, vimelea au vitu vya kemikali husababisha zaidi ya magonjwa 200?

* Makadirio ya hivi karibuni yanaonesha kuwa athari za chakula kisicho salama hugharimu uchumi wa chini na wa kati karibu dola za Kimarekani bilioni 95 katika uzalishaji unaopotea kila mwaka?

* Mienendo bora ya usafi katika sekta ya chakula na kilimo husaidia kupunguza kuibuka na kuenea kwa magonjwa yanayosababishwa na vyakula?

Usalama wa chakula una jukumu muhimu katika kuhakikisha kuwa chakula kinabaki salama katika kila hatua ya mnyororo wa chakula - kuanzia uzalishaji hadi kuvuna, usindikaji, uhifadhi, usambazaji, njia yote hadi maandalizi na matumizi.

Msichana na mvulana waliovaa sare za shule wamesimama kwenye bustani ya shule, kila mmoja akiwa amebeba rundo kubwa la mchicha uliovunwa hivi karibuni.
© WFP/Claudia Altorio Mradi wa ‘mifumo jumuishi ya chakula’ nchini Namibia unaangazia lishe bora na salama, na mbinu bora za ukulima katika mashule kama sehemu ya mpango wa kulisha watoto shuleni unaoungwa mkono na WFP.

Serikali zifanye nini kuhakikisha usalama wa chakula?

Ili kukabiliana na tatizo hili, FAO imependekeza kwamba serikali zianzishe na kusimamia mipango ya kitaifa ya kukabiliana na dharura ya usalama wa chakula, zihakikishe kuna njia iliyoratibiwa katika mashirika ya serikali na mamlaka ya kitaifa ikijumuisha taratibu za kupashana habari haraka pindi matukio ya usalama wa chakula yanapotokea, na kutoa taarifa sahihi na za wazi kwa washika dau wakati wa matukio ya usalama wa chakula na uripoti dharura za kimataifa kwa mtandao wa mamlaka ya kimataifa ya usalama wa chakula (INFOSAN).