Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chakula kichafu chauguza mtu 1 kati ya 10 duniani- FAO/WHO

Familia nchini Syria ikila mkate uliookwa kwa jiko na unga kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP
© UNDP Syria
Familia nchini Syria ikila mkate uliookwa kwa jiko na unga kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo duniani, UNDP

Chakula kichafu chauguza mtu 1 kati ya 10 duniani- FAO/WHO

Afya

Hebu fikiria kila mwaka mtu 1 kati ya 10 huugua baada ya kula chakula kisicho salama! Hizo ni takwimmu zilizotolewa siku ya leo ambayo ni maadhimisho ya 4 ya siku ya kimataifa ya usalama wa chakula duniani.

Mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa, lile la chakula na kilimo, FAO na afya ulimwenguni, WHO ndio yanaratibu siku hii ambayo maudhui yake ni Chakula Salama, Afya Bora, yanalenga kuangazia ya kwamba chakula ni muhimu kwa afya binadamu na ustawi wake, chakula kisipokuwa salama basi malengo ya lishe hayawezi kufikiwa.

Dkt. Simone Moraes Raszl, kutoka Idara ya Usalama wa chakula, WHO amewaeleza waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kuwa, “kiwango cha usalama wa chakula kinapokuwa bora, tunapunguza njaa, utapiamlo na vifo vya watoto wachanga. Utoro wa watoto shuleni unapungua.”

Amesema ndio maana WHO na FAO wanasaidia nchi wanachama katika juhudi za kupatia wananchi wake wote chakula salama na kuwezesha wananchi kula chakula salama ili kulinda afya zao.

Chakula kimeiva na Naomi amepika wali kwa mayai ya kukaanga.
WFP/ Andy Wiggins
Chakula kimeiva na Naomi amepika wali kwa mayai ya kukaanga.

Mathalani tarehe 27 mwezi uliopita wa Mei, Baraza Kuu la WHO lilipitisha mkakati ulioboreshwa wa usalama wa chakula duniani, ikiwa ni miaka 20 baada ya ule wa kwanza. “Mkakati huo unalenga kuimarisha mifumo ya kitaifa ya usalama wa chakula, kusaidia mipango ya sekta mtambuka na mikakati bunifu ya afya ya umma,” amesema Dkt. Raszl.

Hakuna uhakika wa chakula kama chakula si salama

Naye Afisa kutoka FAO akizungumza kwenye mkutano huo amesema katu hakutakuweko na uhakika wa chakula bora na chenye lishe iwapo chakula hicho si salama.

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva, Uswisi, Afisa Mwandamizi wa FAO kuhusu usalama wa chakula Dkt. Markus Lipp, amesema chakula kama si salama hicho siyo chakula kwa sababu kinaweza kusababisha magonjwa na vifo.

Hivyo amesema, “na mvurugano wa sasa wa upatikanaji chakula duniani ambao tumesikia, usalama wa chakula unatakiwa kupatiwa umakini zaidi, maana haiwezekani chakula kilichoko kisababishie watu magonjwa. Malengo ya maendeleo endelevu hayatafikiwa kama chakula si salama.”

FAO inafanya nini?

1. Uhakika wa kupatikana kwa chakula

FAO inashirikiana na serikali duniani kote kusaidia kuhakikisha kuna chakula cha kutosha na chakula kilicho salama na lishe bora. Mathalani nchini Malawi mwaka 2020 hadi 2022, FAO inasaidia kuimarisha mfumo wa kitaifa wa udhibiti wa chakula kwa kushirikiana na serikali, sekta ya chakula wakiwemo wazalishaji wadogo, wasindikaji wa vyakula na vyama vya walaji. Mradi ulilenga katika kutunga sera ya taifa ya usalama wa chakula, ili kuwezesha uzalishaji wa chakula salama.

Wanafunzi wakipatiwa mlo shuleni kaskazini mwa Uganda
UNICEF/Francis Emorut
Wanafunzi wakipatiwa mlo shuleni kaskazini mwa Uganda

2. Biashara

FAO inasaidia nchi kurahisisha biashara kwa misingi ya viwango vilivyokubaliwa kimataifa. FAO ilipoanza kutekeleza mradi wa usimamizi wa mnyororo wa bidhaa za mifugo nchini Thailand mwaka 2015, sekta hiyo ilikuwa hatarini kukumbwa na changamoto za usalama wa chakula kutokana kukosekana kwa mifumo ya ufuatiliaji. Hivi sasa kuna miongozo imeandaliwa na inasaidia kushughulikia dharura za usalama wa chakula

3. Kupunguza usugu wa vijiumbe maradhi vitokanavyo na uchafu kwenye chakul

Kwa msaada kutoka Korea Kusini, FAO imeanza kushirikiana na nchi 6, Bolivia, Cambodia, Colombia, Mongolia, Nepal na Pakistan kupunguza usugu wa vijiumbe maradhi kwa kupitisha viwango vipya vya usimamizi wa  vyakula vinavyoagizwa kutoka nje. Hii inasaidia kulinda walaji dhidi ya vitisho vya kimataifa vya vyakula visivyo salama na kusaidia kuimarisha uwezo wa wazalishaji kufikia masoko ya kimataifa.