Leo ni siku ya kimataifa ya siku ya chakula duniani ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la chakula na kilimo, FAO linasema usalama wa chakula ni muhimu sana kwa sababu chakula kisicho salama ni hatari kwa maisha ya binadamu.
Usalama wa chakula unaanzia shambani hadi kwa mlaji. Kila mwaka watu 600,000 huugua kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao hao 420,000 hufariki dunia.
Chakula kisicho salama ni kipi?
FAO inadadavua zaidi takwimu hizo na kusema ni sawa na mtu 1 kati ya 10 ambao hufariki dunia kila mwaka kutokana na chakula kisicho salama kutokana na kuwa na vimelea, bakteria, virusi, kemikali na aina nyingine zozote za wadudu.
Waathirika wakuu ni makundi yaliyo hatarini kama vile wajawazito, watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano, wazee na watu wenye kinga pungufu ya mwili.
Kwa kutambua hatari hiyo, FAO inasema kila mtu pale nyumbani kwake aliko anaweza kusaidia kupunguza mzigo wa magonjwa na vito vitokanavyo na ulaji wa chakula kisicho salama.
Faida za chakula salama kwa mtoto na mtu mzima
Chakula salama kinasaidia mtoto kukua kwa afya njema; kunaongeza mahudhurio shuleni na tija kazini pindi mtoto anapokuwa mtu mzima, halikadhalika kunapunguza gharama za matibabu.
Chakula salama pia huongeza mahudhurio kazini na kipato kwa watu wazima huku ikipunguza gharama za kutunza wagonjwa; husaidia pia kula virutubisho na pia afya bora kwa muda mrefu.
Je sasa ukiwa nyumbani ufanye nini?
1. Usafi
Nawa mikono yako kwa maji na sabuni kabla ya kuanza mapishi na kila wakati unapokuwa unaendelea na mapishi. Wadudu wanaweza kuhama kwa urahisi kutoka kwenye mikono hadi kwenye chakula wakati wa maandalizi ya chakula. Eneo la kuandalia chakula, mfano kibao cha kukatia mboga na nyama lazima kisafishwe mara kwa mara.
2. Tenganisha
Hakikisha unatenganisha chakula kibichi na kilichopikwa. Mfano nyama mbichi kama vile kuku, samaki, mayai vinaweza kusambaza magonjwa yatokanayo na bakteria kwenye chakula kilichokwishaiva. Kibao cha kukatia nyama, kwa mfano, katu kisitumiwe tena kukatia matunda au kachumbari kabla ya kusafishwa kwa kina. Njia bora zaidi ni kuwa na vibao vya kukatia nyama au mboga vyenye rangi tofauti ili kuweza kutofautisha kwa urahisi.
3. Pika kwa kina
Pika chakula hadi kiive kwa kuzingatia kiwango cha joto kinachopendekezwa na wataalamu. Mathalani nyama, kuku, mayai na samaki vinapaswa viive vizuri. Unapotumia kipima joto cha mapishi jikoni hakikisha unatumbukiza kwenye eneo nene zaidi la chakula chako ili kuhakikisha kinaiva kwa kina.
Hakikisha kipima joto kinasafishwa kwa kina baada ya kutumika. Kama huna kipimajoto unaweza kutambua chakula kimeiva kwa kutazama rangi au kuangalia kiwango cha kulainika.
4. Hifadhi katika joto linalotakiwa
Hakikisha chakula kinahifadhiwa katika kiwango cha joto kinachotakiwa. Bakteria wanaosababisha sumu kwenye chakula huongezeka maradufu na haraka katika kiwango cha joto cha cha chini ya nyuzi joto 5 na zaidi ya nyuzi joto 60.
5. Ubaridi na Joto
Weka chakula kwenye ubaridi haraka na kwa ufasaha. Ikiwezekana andika tarehe ya siku uliyohifadhi chakula kiwe kibichi au kilichopikwa.
6. Mboga na matunda
Osha matunda na mboga kwa kutumia maji safi kabla ya kula.
7. Tumia vyombo visafi
Tumia vyombo visafi kupikia na safisha maeneo ya kuandalia chakula. Unaweza kuchanganya mililita 5 za ujazo za dawa ya kutakatisha vyeupe au ‘bleach’ na mililita za ujazo 750 za maji ili kupata mchanganyiko wa kusafishia maeneo ya kuandalia chakula pamoja na kutakatisha vyombo. La kama hilo haliwezekani, tumbukiza vyombo kwenye maji yanayochemka.