Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takribani watu milioni 1.6 huugua kila siku kutokana na chakula kisicho salama: WHO

Wanawake wakiandaa mboga wakati wa hafla ya kujifunza njia bora za kuzuia NCDs kama vile lishe, huko Tulagi, Visiwa vya Solomon.
© WHO/ Blink Media/Neil Nuia
Wanawake wakiandaa mboga wakati wa hafla ya kujifunza njia bora za kuzuia NCDs kama vile lishe, huko Tulagi, Visiwa vya Solomon.

Takribani watu milioni 1.6 huugua kila siku kutokana na chakula kisicho salama: WHO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Ikiwa leo ni Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula, Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Ulimwenguni WHO limeripoti kwamba kila siku, takribani watu milioni 1.6 kote duniani huugua kwa kula chakula kisicho salama na karibu asilimia 40 ya mzigo huo ukibebwa na watoto wadogo, chini ya umri wa miaka mitano. 

Hii leo kupitia mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari jijini Geneva, Uswisi uliowahusisha Dkt. Francesco Branca, Mkurugenzi wa Idara ya Lishe na Usalama wa Chakula wa WHO na Markus Lipp, Afisa Mwandamizi wa Usalama wa Chakula wa FAO imeelezwa kuwa madhara yatokanayo na chakula kisicho salama hayaangalii mipaka na yametapakaa katika nchi nyingi duniani.  

Dkt. Francesco Branca aliyekuwa katika ukumbi huo wa mikutano ametoa taarifa kwamba "kutokana na kuugua kwa takribani watu milioni 1.6 kila siku kunakosababishwa na vyakula visivyo salama, (kila mwaka) watu 420,000 hufariki dunia kutokana na sababu hiyo."

Mwaka huu, kaulimbiu ya kampeni ya Siku ya Kimataifa ya Usalama wa Chakula, ni Jiandae kwa Yasiyotarajiwa, ambayo sio tu inasisitiza umuhimu wa kuwa tayari kudhibiti matukio ya usalama wa chakula ili yasiwe ya dharura, lakini pia umuhimu wa kuchukua muda kupanga, kuandaa na kuwa tayari kuchukua hatua katika mazingira ya dharura.

Kwa upande wake Markus Lipp, Afisa Mwandamizi wa Usalama wa Chakula katika Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), kwa njia ya video akizungumza kutoka Roma, Italia ameeleza namna FAO inavyohusisha chakula salama na utimizaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu…anasema, “Chakula kinapozalishwa na kuuzwa katika mfumo wa kilimo salama na endelevu, kinachangia maisha yenye afya na kuboresha uendelevu kwa kuwezesha upatikanaji wa soko na tija, ambavyo vinasukuma maendeleo ya kiuchumi na kupunguza umaskini, hasa katika maeneo ya vijijini.”