Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan Kusini: UNMISS yaendeleza utulivu kufuatia kuzuka kwa vurugu huko Malakal

Watu wakiwa foleni katika eneo la usambazaji wa chakula huko Malakal, Sudan Kusini.
© WFP/Eulalia Berlanga
Watu wakiwa foleni katika eneo la usambazaji wa chakula huko Malakal, Sudan Kusini.

Sudan Kusini: UNMISS yaendeleza utulivu kufuatia kuzuka kwa vurugu huko Malakal

Amani na Usalama

Kufuatia kuzuka kwa ghasia wiki iliyopita huko Malakal, jimbo la Upper Nile, nchini Sudan Kusini, Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini UNMISS unaendelea kuunga mkono juhudi za kulinda raia na kudumisha utulivu kupitia doria kali na kuendeleza kuwasiliana kwa karibu na jamii zilizoathirika na ghasia hizo.

Taarifa iliyotolewa leo na UNMISS kutoka jijini Juba nchini humo imepongeza hatua za haraka zilizochukuliwa na mamlaka ya serikali pamoja na vikosi vya usalama vya serikali na kupunguza mivutano na kuweka jamii salama. 

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ambaye pia ni na Mkuu wa UNMISS Nicholas Haysom, amesema hali kwa saa ni shwari lakini tete "Tunashukuru uratibu na ushirikiano wa karibu na mamlaka za kitaifa, serikali na serikali za mitaa ambazo zilichukua jukumu muhimu katika kuhakikisha kwamba hakuna ongezeko zaidi la vurugu na kwamba watu wanaweza kuendelea na shughuli zao za kila siku kwa usalama," 

Ujumbe huo unafanya kazi kwa karibu na serikali pamoja na wadau na umetuma askari wa kulinda amani ndani na karibu na eneo la Umoja wa Mataifa la Ulinzi wa Raia huko Malakal ili kuhakikisha kuwa watu waliokimbia makazi yao wako salama.