Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF: Kuna ongezeko la ukatili kwa 30% dhidi ya watoto DRC

Balozi mwema wa UNICEF Orlando Bloom akimsalimia mtoto wakati alipotembelea eneo la Bushagara kwa wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Balozi mwema wa UNICEF Orlando Bloom akimsalimia mtoto wakati alipotembelea eneo la Bushagara kwa wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

UNICEF: Kuna ongezeko la ukatili kwa 30% dhidi ya watoto DRC

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa umethibitisha kuna ongezeko la karibia asilimia 30 ya ukatili dhidi ya Watoto katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC kwa kipindi cha miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu ukilinganisha na robo ya mwaka 2023.

Taarifa iliyotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF kutoka Goma nchini DRC na New York nchini Marekani imeeeleza kuwa ongezeko la ghasia na kuhama kwa watu kutoka katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo kumepelekea kuibuka kwa ukiukwaji mkubwa dhidi ya Watoto. 

UNICEF pia wameeleza kuhusu ziara ya Balozi mwema wa shirika hilo Bwana Orlando Bloom ambaye ametembelea DRC na kuzuru maeneo mbalimbali zikiwepo kambi za wakimbizi, maeneo salama ya Watoto Pamoja na kuzungumza na waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia. 

Balozi wa Nia Njema Orlando Bloom akutana na waandishi wa habari watoto na wajumbe wa kamati za watoto kwa eneo salama la watoto katika eneo la Bulengo kwa wakimbizi wa ndani huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Balozi wa Nia Njema Orlando Bloom akutana na waandishi wa habari watoto na wajumbe wa kamati za watoto kwa eneo salama la watoto katika eneo la Bulengo kwa wakimbizi wa ndani huko Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akieleza aliyoshuhudia katika ziara yake Bwana Bloom amesema “Kiwango cha kushangaza cha mzozo mashariki mwa DRC, kiwango cha kutisha cha ghasia, na athari zake mbaya kwa watoto na wanawake niliokutana nao ni ya kuumiza moyo, hakika hakuna mtoto anayestahili kuishi katika mazingira magumu kama jinsi nilivyoona katika kambi ya wakimbizi wa ndani ambao wametengwa na familia zao bila matumaini ya kwenda shuleni na hasa wakiwa kwenye hatari zaidi ya kukumbana na hatari ya kudhulumiwa kingono”.

Akiwa katika ziara yake katika hospitali ya Panzi, Bloom alikutana na manusura wa unyanyasaji wa kijinsia “Hadithi zinazosimuliwa na wasichana na wanawake walionusurika na ukatili wa kijinsia zinaumiza sana, lakini katikati ya maumivu wanayoyapitia mimi nimefikiria tofauti kuwa kuna haja kubwa ya kutoa msaada wa kibinadamu ikiwemo huduma za afya, msaada wa kisaikolojia na msaada wa kisheria ili kuwasaidia walionusurika kupata nguvu  na kujenga tena maisha yao, na mengine zaidi yafanyike ili kuwalinda wasichana na wanawake dhidi ya ukatili”.

UNICEF katika taarifa hiyo pia wameeleza kuwa imethibitishwa kuna kesi zaidi ya 1000 za ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto katika majimbo matatu ya mashariki ya Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini katika robo ya kwanza ya mwaka huu. Hii inawakilisha ongezeko la asilimia 30 ikilinganishwa na robo ya mwisho ya 2023, huku suala la kuajiri na kutumikisha watoto kumekua kwa kasi zaidi. Hata hivyo, Mnamo mwezi Aprili 2024, kumekuwa na kesi zaidi ya 450 zilizo thibitishwa za ukiukwaji mkubwa dhidi ya watoto huko mashariki mwa DRC.

Unyanyasaji wa kijinsia na migogoro ya kijinsia dhidi ya wanawake na watoto imebaki kuwa mikubwa katika mwaka 2023 na kunaongezeka zaidi kwa mwaka 2024 huku unyanyapaa na woga wa kulipiza kisasi ukizuia waathirika wengi kujitokeza hadharani. 

Balozi mwema wa UNICEF Orlando Bloom akimpatia mtoto uji katika kituo cha lishe kinachoungwa mkono na UNICEF katika eneo la Bushagara kwa wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
© UNICEF/Vincent Tremeau
Balozi mwema wa UNICEF Orlando Bloom akimpatia mtoto uji katika kituo cha lishe kinachoungwa mkono na UNICEF katika eneo la Bushagara kwa wakimbizi wa ndani mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Katika eneo la mashariki mwa DRC, takribani watu milioni 5, ikiwemo watoto milioni 2.8 wanahitaji misaada ya haraka ya kibinadamu kutokana na kuongezeka kwa tatizo hili, hata hivyo UNICEF inaendelea kuboresha elimu, afya na kutoa msaada wa ulinzi kwa watoto, wanawake na familia zilizoathirika na vita. 

"Kila siku, watoto na wanawake katika kambi za wakimbizi za DRC wanakabiliwa na matatizo makubwa. Mahitaji yao ni makubwa, na mwitikio wa mgogoro unapungua. Ni lazima tuungane kwa haraka ili kuhakikisha wanaishi kwa usalama na heshima,” alisema Boom baada ya kutembelea kambi ya wakimbizi wa ndani.

UNICEF imeendelea kurejea tena wafadhili kuwapatia msaada unaohitajika kwani ombi la kibinadamu la dola za milioni 804.3 linafadhiliwa kwa asilimia 10 pekee.