Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kila mtu ana wajibu wa kuhusika na urejeshaji wa ubora wa ardhi: UN

Mtoto akiwa mbele ya shule yake katika eneo la Somalia nchini Ethiopia
© UNICEF/Raphael Pouget
Mtoto akiwa mbele ya shule yake katika eneo la Somalia nchini Ethiopia

Kila mtu ana wajibu wa kuhusika na urejeshaji wa ubora wa ardhi: UN

Tabianchi na mazingira

Leo ni siku ya mazingira duniani na Umoja wa Mataifa unaisa dunia kuchukua hatua sasa kurejesha Uhai wa ardhi iliyoharibiwa na kujenga mnepo dhidi ya kuongezeka kwa hali ya jangwa na ukame na hiyo ndio kaulimbiu ya siku ya mwaka huu.

Akisisitiza maudhui hayo Inger Andersen Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP amemtaka kila mtu kujiunga na harakati za kimataifa za kurejesha ardhi yenye afya na kujenga mnepo wa majanga mengine kama vile ukame na hali ya jangwa.

Anasema “Kwa sababu  uharibifu wa ardhi na kuenea kwa jangwa huathiri zaidi ya watu bilioni tatu duniani. Mifumo ya ikolojia ya maji safi pia imeharibika, hivyo kufanya kuwa vigumu kupanda mazao na kufuga mifugo. Hii inawaathiri vibaya wakulima wadogo na, bila shaka, maskini wa vijijini.”

Mashirika ya UN yana fursa nzuri kutekeleza hilo

Kwa kutambua changamoto hiyo mashirika mengi ya Umoja wa Mataifa na wadau wanachukua hatua kuhakikisha athari zinapungua hasa kwa wakulima wadogo matahalani Sulawesi nchini Indonesia ambako mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo IFAD unawashika mkono wakulima wadogo wa mpunga na kakao kwa mafunzo ya mbinu bora za kilimoikiwemo kutumia mbolea asilia ili kulinda rytba ya ardhi, kuongez mavuno na kuinua kipato.

Boiman ni miongoni mwa wakulima hao analima mpunga na kakao “Nimekuwa mkulima tangu utoto wangu nikiwa na umri wa miaka 10 tu, lakini kwa muda wote huo sikujua ufundi na taratibu zinazohitajika kuwa mkulima bora. Wakati wa msimu wa ukame miti yangu ya kakao yote ilikauka na ndipo nilipojaribu mbolea asilia mwezi Novemba na matokeo kwa muda mfupi yakama mazuri sana.”

Ili kupata mbolea hiyo ya asili amepewa mafunzo ya kuitengezena na IFAD ambapo anachanganya majani, mabaki ya mkaa, mkojo na kinyesi cha ng’ombe na kisha anachanganya na fangasi asilia wa Trichoderma na kuachwa mchanganyiko huo hadi uchache kwa muda wa mwezi mmoja ili kutengeneza mboji yenye rutuba.

Na kwa kufanya hivyo Boiman anasema “Hivi sasa udongo wa mashamba yangu una rutba na afya na unaimarika kila mwaka.”

Boiman mbali ya kuitumia mboji hiyo katika mashamba yake anaiuza pia kwa wakulima wenzake na kujiongezea kipato kuinua uchumi wa familia. Huku IFAD ikilenga kuwafikia wakulima wadogo zaidi ya 340,000 na mradi huo.

Urejesheji wa afya ya ardhi ndio nguzo ya mustakbali wa dunia

Bi. Andersen amesisitiza kuwa “Urejeshaji wa ardhi unaweza kuwa uzi wa dhahabu wa kuunganisha pamoja hatua na matarajio Kwa hivyo ni lazima tuifanye kazi hii iwe na maana. Katika siku hii muhimu, ninaomba kila mtu ajiunge na kizazi cha urejeshaji. Ardhi yetu ni mustakabali wetu na lazima tuilinde.”

Na uwekezaji wa aina hi indio umesisitizwa pia na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake akisema ““Kutochukua hatua ni gharama kubwa. Lakini hatua za haraka na zenye ufanisi zinaleta maana ya kiuchumi kwani Kila dola iliyowekezwa katika urejeshaji wa mfumo wa ikolojia hutengeneza hadi dola thelathini katika manufaa ya kiuchumi.”