Kila sekunde tano hewa chafuzi inachukua uhai wa mtu duniani

3 Juni 2019

Kuelekea siku ya mazingira duniani, tarehe 5 mwezi  huu wa Juni, mtaalamu huru wa Umoja wa Mataifa amesihi serikali duniani zichukue hatua kuondokana na uchafuzi wa hali ya hewa kama wajibu wao wa kutekeleza haki za binadamu.

Mtaalamu huyo David Boyd ambaye anahusika na haki za binadamu na mazingira amesema hayo kupitia taarifa iliyotolewa leo huko Geneva, Uswisi na ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa.

“Uchafuzi wa hewa ni muuaji wa taratibu, asiyeonekana na anahusika na vifo vya mapema vya watu milioni 7 kila mwaka, wengi wao wakiwa ni wanawake, na watoto na jamii maskini,” amesema Bwana Boyd akiongeza kuwa takwimu hizo ni sawa na mtu kufariki dunia kila baada ya sekunde tano.

Amesema kwamba kushindwa kuhakikisha uwepo wa hewa safi ni kinyume na haki ya binadamu ya uhai, afya na ustawi pamoja na haki ya kuishi katika mazingira yenye afya.

Kwa mantiki hiyo amesema, “serikali lazima zichukue hatua za dharura kuboresha kiwango cha hali ya hewa na kwa kufanya hivyo zitakuwa zinatimiza wajibu wao wa  haki za binadamu.”

Amesisitiza kuwa haki ya mazingira yenye afya ni msingi wa ustawi wa binadamu na inatambuliwa na zaidi ya mataifa 150 katika ngazi ya taifa na kikanda hivyo amesema, “haki hii inapaswa kupatiwa msisitizo kimataifa ili kuhakikisha haki hii inafurahiwa na kila mtu, popote alipo huku misingi ya haki za binadamu duniani na kutokubaguliwa ikizingatiwa.”

Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.
© UN-Habitat /Julius Mwelu
Saruji ya ujenzi wa majengo nayo inachangia katika uchafuzi wa hewa ya ukaa kutokana na jinsi ambavyo inazalishwa.

Mtaalam huyo ametoa mfano wa simulizi za mafanikio  katika udhibiti wa hewa chafuzi akitaja China  ambayo mwaka huu ndio mwenyeji wa siku ya mazingira duniani.

Mwaka 1998, mji mkuu wa China, Beijing ulianza mipango madhubuti ya kukabiliana na uchafuzi wa  hali ya hewa na katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Beijing, imetekeleza hatua kadhaa ikiwemo kuboresha miundombinu ya usafiri na kuweka vidhibiti hewa chafuzi kwenye magari na kati ya mwaka 2013 hadi 2017 kiwango cha chembechembe za hewa chafuzi Beijingi  kimepungua kwa asilimia  35 mjini humo na asilimia 25 maeneo ya jirani.

Amesema simulizi za mafanikio ni ushahidi tosha kuwa uchafuzi wa hewa ni tatizo ambalo linaweza kuzuillika.

Ametaja hatua saba muhimu ambazo serikali zinapaswa kuchukua ambapo mosi ni kufuatilia viwango vya hewa na madhara yake kiafya, pili; kutathmini vyanzo vya uchafuzi wa hewa; tatu kupatia umma taarifa kuhusu ushauri wa afya ya umma; nne kuanzisha sheria, sera na kanuni kuhusu viwango vya ubora wa hewa; tano; kuandaa mipango ya mashinani kuhusu viwango vya ubora wa hewa; sita ni kutekeleza mipango hiyo na saba ni kutathmini maendeleo ya utekelezaji kuhakikisha viwango vinazingatiwa.

 

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter