Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tuna dunia moja pekee, tunapaswa kuilinda- Guterres

Ngozi ya Samaki inatumika katika tasnia ya mitindo.
Video Capture/Unifeed
Ngozi ya Samaki inatumika katika tasnia ya mitindo.

Tuna dunia moja pekee, tunapaswa kuilinda- Guterres

Tabianchi na mazingira

Tarehe 5 mwezi Juni kila mwaka ni siku ya mazingira duniani maudhui yakiwa ni “Dunia Moja Pekee” ikimaanisha kuwa hakuna pa kukimbilia iwapo dunia hii itachafuliwa,

Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.
UNDP/Ngele Ali
Familia za Turkana zinatumia kilimo cha umwagiliaji kulima mazao ya chakula wakati wa ukame wa muda mrefu nchini Kenya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku ya leo anasema “ni maneno machache yaliyobeba ujumbe mzito na halisia.”

Anasema sayari dunia ndio makazi yetu pekee, “ni muhimu kulinda afya ya anga lake, utajiri, na aina mbalimbali ya viumbe vilivyoko duniani bila kusahau ikolojia yake na rasilimali lukuki.”

Guterres anasema “lakini tunashindwa kufanya hivyo. Tunaibebesha dunia mzigo mkubwa wa kujilinda kwa njia ambayo si endelevu. Mifumo asili ya dunia haiwezi kuenda na kasi ya matakwa yetu.”

Afya ya sayari dunia si faida kwa dunia peke yake

Kinachoharibika si dunia pekee, bali binadamu pia wanadhurika. Mazingira yenye afya ni muhimu kwa ajili ya watu wote na kwa ajili ya malengo 17 ya maendeleo endelevu, SDGs.

Katibu Mkuu anesema mazingira yenye afya, “hutupatia chakula, maji safi, dawa, na hurekebisha hali za kupitiliza za tabia nchi, halikadhalika huepusha majanga makali ya hali ya hewa,”

Ni kwa mantiki hiyo Guterres anasema ni muhimu sana kusimamia kwa ukamilifu mazingira na kuhakikisha huduma zake zinafikia pia watu wote hususan jamii zilizo hatarini zaidi.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.
Screenshot
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, jamii ya wafugaji, Maasai wa Loliondo kaskazini mwa Tanzania wamelazimika kuhamia katika kilimo.

Takwimu zinasemaje?

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya watu bilioni 3 wameathiriwa na kumomonyoka kwa mifumo ya ikolojia.

Uchafuzi wa hewa unasababisha watu milioni 9 kufariki dunia kutokana kabla ya kutimiza umri wa miaka 75, au YPLL kwa kiingereza.

Na kwa mimea na baadhi ya aina za wanyama viko hatarini kutoweka ndani ya miongo michache.

Takribani nusu ya wakazi wa dunia wako katika hatari ya kuathiriwa na mabadiliko ya tabianchi—sawa na mara 15 zaidi ya kufa kutokana na madhara ya mabadiliko ya tabianchi kama vile joto kupindukia, mafuriko na ukame.

Azimio la miaka 50 huko Stockholm, Sweden mashakani

Miaka 50 iliyopita viongozi wa nchi walikutana Sweden wakati wa mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira ya binadamu, na kuahidi kulinda sayari dunia, “lakini tuko mbali sana kufanikisha azimio hilo,” amesema Guterres akiongeza kuwa, “hatuwezi kuendelea kupuuza kengele ambayo inalia kwa sauti kubwa kila uchao.”

Kiwanda hiki cha samaki cha Butyaba kimefungwa baada ya kutwama kwenye maji yatokanayo na ongezeko la maji katika Ziwa Albert.
UN/ John Kibego
Kiwanda hiki cha samaki cha Butyaba kimefungwa baada ya kutwama kwenye maji yatokanayo na ongezeko la maji katika Ziwa Albert.

Mwelekeo unaohitajika

Serikali lazima zipatie kipaumbele hatua kwa tabianchi na kulinda mazingira kwa kutumia sera sahihi ambazo zinasongesha maendeleo endelevu.

Sekta ya biashara ihakikishe uendelevu ndio kitovu cha maamuzi yao kwa maslahi ya binadamu na dunia. “Sayari yenye afya ni uti wa mgongo wa kila sekta duniani.”

Wapiga kura nao na walaji lazima wachukue hatua zinazoleta mabadiliko chanya: “kuanzia sera wanazounga mkono, aina ya chakula tunachokula, usafiri tunaochagua, kampuni tunazounga mkono. Sote tunaweza kuweka mazingira safi kutokana na maamuzi yetu tunayochagua.”

Mkoba uliotengenezwa kutokana na ngozi ya Samaki
Video Capture/Unifeed
Mkoba uliotengenezwa kutokana na ngozi ya Samaki

Wanawake na wasichana nao wasiachwe nyuma kwa kuwa wanaweza kuwa mawakala thabiti wa mabadiliko, amesema Guterres bila kusahau maarifa ya kijadi na yale ya jamii za kiasili.

Amesema Umoja wa Mataifa kwa upande wake umejizatiti kusongesha ushirikiano wa pamoja duniani kwa sababu njia pekee ni kushirikiana na asili badala ya kuipinga asili. “Kwa pamoja tunaweza kuhakikisha sayari yetu siyo tu inasalia bali pia inachafua kwa sababu tuna Dunia Moja Pekee.”