Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAITI: WFP yafikisha misaada kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa Port-au-Prince

Ndege ya mizigo ya WFP katika uwanja wa ndege wa Port-au-Prince ikiwa na vifaa muhimu vya matibabu kwa wale wanaohitaji zaidi nchini Haiti.
© WFP/UNHAS
Ndege ya mizigo ya WFP katika uwanja wa ndege wa Port-au-Prince ikiwa na vifaa muhimu vya matibabu kwa wale wanaohitaji zaidi nchini Haiti.

HAITI: WFP yafikisha misaada kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa Port-au-Prince

Msaada wa Kibinadamu

Hatimaye wakazi wa kitongoji cha Cité Soleil kwenye mji mkuu wa Haiti, Port-au-Prince wataanza kupata mlo baada ya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP kufikisha shehena za vyakula, eneo ambalo mwishoni mwa mwaka 20222 lilitajwa kugubikwa na kiwango cha juu zaidi cha njaa.

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo huko Port-au-Prince inasema pamoja na shehena hizo za vyakula kuingia, wameweza pia kutumia uwanja wa ndege wa kimataifa wa mji huo mkuu kwa ajili ya ndege zinazotoa huduma za kibinadamu na pia ndege za mizigo. 

Ndege ya mizigo iliyokodishwa na WFP ilitua uwanja huo wa ndege wa kimataifa wa Port-au-Prince Alhamisi iliyopita ya tarehe 30 mwezi Mei ikiwa na vifaa vya matibabu kwa ajili ya mashirika yanayotoa misaada Haiti. 

Hiyo ni ndege ya kwanza ya Umoja wa Mataifa kutua eneo hilo tangu ghasia zianze mwezi Machi mwaka huu wa 2024. 

“Licha ya hali ngumu ya usalama, WFP inachukua hatua muhimu za awali za kiutu za kusambaza misaada ya kibinadamu kama vile chakula kwa wale wenye uhitaji mkubwa zaidi kwenye vitongoji vya Port-au-Prince,” amesema Jean-Martin Bauer, Mwakilish Mkazi wa WFP nchini Haiti. 

Bandari nazo zifunguliwe tufikishe misaada zaidi

“Maendeleo haya yanapaswa pia kufanyika kwenye bandari zote mjini Port-au-Prince, bandari ambazo bado zinakumbwa na hali  tete ya usalama. Bila uwepo wa njia za uhakika na endelevu za kufikisha misaada ya kiutu na kufunguliwa kwa njia muhimu za kugawa misaada, watu wako hatarini kutumbukia kwenye njaa kali,” ameonya Bwana Bauer.

Shirika la Ndege la Umoja wa Mataifa la kutoa huduma za kiutu, UNHAS nalo limeanza safari za abira kuelekea uwanja huo wa ndege ambao ulifungwa mwezi mapema mwezi Machi kutokana na ukosefu wa usalama. 

Wanufaika Cité Soleil wapata chakula na fedha taslimu

Katika kipindi cha wiki mbili za mwezi Mei, zaidi ya tani za ujazo 615 za mchele, maharage, mafuta ya kupia yalisambazwa kwa takribani watu 93,000 huko Cité Soleil, wakiwemo wanawake wanaonyonyesha watoto na watoot ambao walikosa msaada ukutokana na ghasia mpya kwenye mji mkuu Port-au-Prince. 

WFP pia imetoa mgao wa fedha taslimu wa jumla yad ola milioni 8 kwa watu walio katika dharura, vile vile kwa ajili ya mpango wa kujenga mnepo na pia hifadhi ya kijamii.