Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukata walilazimu WFP kupunguza watu wnaopokea msaada wa chakula Haiti

Watoto wa shule nchini Haiti wakipata  mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.
© WFP/Jonathan Dumont
Watoto wa shule nchini Haiti wakipata mlo kupitia programu ya mlo shuleni inayotolewa na shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani, WFP nchini humo.

Ukata walilazimu WFP kupunguza watu wnaopokea msaada wa chakula Haiti

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani WFP, limesema limelazimika kupunguza idadi ya watu wanaopokea msaada wa dharura wa chakula nchini Haiti kwa asilimia 25 mwezi Julai, ikilinganishwa na mwezi uliopita, kutokana na ukata unaolikabili shirika hilo.


 

Kwa mujibu wa shirika hilo “Cha kusikitisha ni kwamba, hii ina maana  kwamba watu 100,000  raia  wa Haiti walio katika mazingira magumu zaidi wanalazimika kuishi bila msaada wowote wa WFP mwezi huu.”

Katika kiwango cha sasa cha ufadhili wa mwaka huu, WFP inakosa rasilimali za kutosha kutoa msaada wa chakula kwa jumla ya watu 750,000 ambao wanahitaji msaada wa haraka.

“Hali hii imekuja wakati ambapo nchi inakabiliwa na kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa cha mahitaji ya kibinadamu, na karibu nusu ya watu  ambao ni watu milioni 4.9  hawawezi kupata chakula cha kutosha.” Limeongeza shirika hilo.

Ombi la msaada limefadhiliwa kwa asilimia 16 tu

Katika miezi sita ya kwanza ya mwaka huu WFP inasema , mpango wa kukabiliana na changamoto za kibinadamu nchini Haiti umefadhiliwa kwa asilimia 16 pekee na shirika hilo linahitaji kwa haraka dola milioni 121 hadi mwisho wa mwaka huu wa 2023 ili kuendelea kutoa msaada muhimu wa kibinadamu nchini humo.

WFP inalenga kufikia watu milioni 2.3 nchini Haiti mwaka 2023 lakini uhaba wa fedha unatishia lengo hilo.

"Inasikitisha kushindwa kuwafikia baadhi ya Wahaiti walio hatarini zaidi mwezi huu. Ukata huu wa fedha umekuja wakati mbaya sana, kwani Wahaiti wanakabiliwa na majanga mbalimbali ya kibinadamu huku maisha yao na riziki zao zikisambaratishwa na vurugu, ukosefu wa usalama, msukosuko wa kiuchumi na majanga ya tabianchi. Tusipopata ufadhili wa haraka, upunguzaji mbaya zaidi msaada wa chakula utaendelea” amesema Jean-Martin Bauer, mkurugenzi wa WFP nchini Haiti.

Msaada uliotolewa hadi sasa

Katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2023, WFP imetoa chakula cha moto shuleni kwa zaidi ya watoto wa shule 450,000 kote nchini.

Kwa wanafunzi wengi, ni mlo kamili pekee wanaokula kwa siku. Bila kuongeza fedha karibu nusu ya watoto hawa hawataweza tena kupata milo ya shule watakaporejea darasani baada ya mapumziko ya kiangazi.

Bwana Bauer amesema "Tunajivunia kile ambacho tumeweza kukifanya kufikia sasa katika 2023, shukrani kwa msaada kutoka kwa wafadhili wetu. Tuna watu, mpango, na uwezo wa kuendelea, lakini kwa wakati huu, bila ufadhili wa haraka, tunalazimika kupunguza msaada hali ambayo inamaanisha maelfu ya Wahaiti walio hatarini zaidi hawatapokea msaada mwaka huu. Huu sio wakati wa kupunguza, ni wakati wa kupiga hatua. Hatuwezi kuwaangusha Wahaiti wakati wanatuhitaji zaidi.”

Licha ya changamoto kubwa, WFP inasema imeongeza shughuli zake ili kukabiliana na kiwango cha mahitaji ambacho hakijawahi kushuhudiwa nchini Haiti tangu tetemeko la ardhi la 2010, kutoa msaada kwa watu milioni 1.5 katika miezi sita ya kwanza ya mwaka.

Mbali na msaada wa chakula, shirika hilo linasema familia zilipokea fecha taslim. Hii inawaruhusu kuamua jinsi wanavyolisha familia zao na kukidhi mahitaji yao ya haraka ya chakula huku pia wakiingiza rasilimali katika uchumi wa ndani. WFP imeongeza maradufu idadi ya wanafunzi wanaopokea milo shuleni inayotengenezwa kutokana na  mazao yanayozalishwa ndani ya nchi.

Lakini upungufu wa ufadhili kwa mujibu wa shirika hilo unamaanisha kuwa faida hizi ziko hatarini.