Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na mradi wa Lishe Bora kwa Wanawake Wajawazito nchini Rwanda

Mama akiwa amembeba mtoto wake nje ya nyumba yake katika Kambi ya Wakimbizi ya Kiziba nchini Rwanda.
© WFP/Emily Fredenberg
Mama akiwa amembeba mtoto wake nje ya nyumba yake katika Kambi ya Wakimbizi ya Kiziba nchini Rwanda.

UNICEF na mradi wa Lishe Bora kwa Wanawake Wajawazito nchini Rwanda

Afya

Nchini Rwanda, hivi karibuni Wizara ya Afya ya nchi hiyo, kupitia Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), imeanza usambazaji wa Vidonge vyenye virutubisho vingi vya lishe (MMS) ili kuboresha lishe ya wajawazito kama njia ya kupunguza kasi ya udumavu kwa watoto.

Nshimiyimana Clementine ni Mkuu wa Kituo cha Afya cha Kabaya, Wilayani Ngororero katika Jimbo la Magharibi nchini Rwanda anasema, “Wajawazito wanapata taarifa kutoka kwa Wahudumu Afya Jamii ambao wanawaelekeza kwenda kwenye vituo vya afya kwa ajili ya vipimo muhimu na kupata vidonge vya lishe.”

“Tunawashauri kumeza kidonge kimoja kila siku angalau kwa miezi sita. Na sasa kwa kuwa tumeanza kusambaza vidonge lishe hivi tunaamini vitakuwa na manufaa kwa kuzingatia lishe zilizomo. Wajawazito hawatakosa virutubisho kutoka kwenye matunda na mbogamboga kwa kuwa hivi vidonge vinavyo. Japo bado tunawahimiza wajawazito kula matunda na mbogamboga, lakini wale wasiomudu hawataathirika na upungufu wa virutubisho. ”

Umugwaneza Yvette ni mmoja wa wajawazito wanufaika wa programu hii iliyowezeshwa kwa ukarimu wa KIRK Humanitarian shirika lisilo la kiserikali linalojitolea kuhakikisha Virutubisho lishe kupitia Umoja wa Mataifa vinawafikia wajawazito kokote waliko duniani.

“Wakati usambazaji wa vidonge vya MMS ulipoanza, nilikuwa miongoni mwa watu wa mwanzo kupokea. Mwili wangu umevipokea vizuri. Sijapata changamoto yoyote. Ninameza mara kwa mara na ninajisikia mwenye afya.”