Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sudan: Mamilioni wakikabiliwa na njaa, wahudumu wa misaada waomba ruhusa ya kufikisha misaada

Watoto wanachota maji safi na salama kutoka kwa kituo kilichosakinishwa na UNICEF katika kijiji cha Al-Serif huko Darfur nchini Sudan.
© UNICEF/Tariq Khalil
Watoto wanachota maji safi na salama kutoka kwa kituo kilichosakinishwa na UNICEF katika kijiji cha Al-Serif huko Darfur nchini Sudan.

Sudan: Mamilioni wakikabiliwa na njaa, wahudumu wa misaada waomba ruhusa ya kufikisha misaada

Msaada wa Kibinadamu

Njaa nchini Sudan “imekaribia sana” ikiwa mashirika ya misaada yataendelea kuzuiwa kutoa msaada, wameonya wahudumu wa misaada wa Umoja wa Mataifa leo Mei 31.

Katika tathmini mbaya ya hali ngumu zaidi nchini Sudan ambapo mgogoro unaingia mwaka wake wa pili, wakuu wa mashirika 19 ya kibinadamu duniani wametoa tahadhari kwamba iwapo kutakuwa na vizuizi zaidi vya kutoa msaada “haraka na kwa wingi” vitamaanisha kwamba “watu zaidi watakufa”.

Msemaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura (OCHA) Jens Laerke ameawaambia waandishi wa habari leo mjini Geneva kwamba njaa “inaweza kushamiri katika sehemu kubwa za nchi, watu zaidi watakimbilia nchi jirani, watoto wataangamia kwa magonjwa na utapiamlo na wanawake na wasichana watakabiliwa na mateso na hatari kubwa zaidi”.

Kiwango cha njaa kinachotisha

Takriban watu milioni 18 nchini humo tayari wanakabiliwa na njaa kali na watoto milioni 3.6 wanakabiliwa na utapiamlo mkali, amesema msemaji wa OCHA.

Watoto hawa wako katika hatari kubwa, Bwana Laerke amesisitiza, kwani “wanakabiliwa na uwezekano wa kufa mara 10 hadi 11 zaidi” kuliko watoto wenye chakula cha kutosha.

Licha ya mahitaji makubwa yanayozidi, wafanyakazi wa misaada wanaendelea kukabiliana na “vikwazo vya kimfumo na kukataliwa kwa makusudi kwa upatikanaji wa misaada na pande zote za mgogoro,” kulingana na taarifa ya pamoja ya mashirika ya kibinadamu.

Hatari kufikia misaada

Bwana Laerke ameelezea kwamba “harakati za kuvuka maeneo ya mgogoro kwenda sehemu za Khartoum, Darfur, Aj Jazirah na Kordofan zimekatwa tangu katikati ya mwezi wa Desemba” na kwamba mnamo Machi na Aprili mwaka huu, takriban watu 860,000 walinyimwa misaada ya kibinadamu katika maeneo haya.

Hali za utoaji misaada ni “mbaya sana na hatari,” ameongeza, akisisitiza kwamba wafanyakazi wa misaada wanauawa, kujeruhiwa na kuhangaishwa, huku vifaa vya misaada vikiporwa.

Isitoshe, kufungwa kwa mpaka wa Adré kutoka Chad hadi Darfur Magharibi mwezi Februari kumepunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa misaada Darfur.

Mafanikio Darfur

Wiki iliyopita, malori ya Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa Duniani (WFP) yaliweza kuingia Sudan kutoka Chad kupitia mpaka wa Tine hali ambayo inatia moyo. Shirika hilo liliripoti kwamba tani 1,200 za chakula kwa ajili ya takriban watu 116,000 zinapelekwa kote katika eneo la Darfur.

Siku ya Ijumaa, Leni Kinzli wa WFP Sudan alithibitisha kwamba misafara iliyokuwa inaelekea Darfur ya Kati (Umshalaya na Rongatas) ilifika maeneno yaliyokusudiwa, ilhali msafara kueelekea maeneo 12 ya Darfur Kusini, ikiwemo kambi za wakimbizi wa ndani Nyala, bado uko safarini.

Wakati huo huo, Bwana Laerke ameonya kwamba katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini El Fasher, ambapo mgogoro kati ya vikosi viwili pinzani Sudanese Armed Forces (SAF) na Rapid Support Forces (RSF), takriban raia 800,000 wanajiandaa kwa “shambulio kubwa linalokaribia”.

Kushambuliwa kutoka pande zote

Jana Alhamisi Mei 30, afisa mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini humo Clementine Nkweta-Salami ameonya kwamba raia “wanashambuliwa kutoka pande zote”.

Amesema kwamba vituo vya matibabu, kambi za wakimbizi wa ndani na miundombinu muhimu ya kiraia katika El Fasher; jimbo la Darfur Kaskazini, vimeshambuliwa na pande zote za mgogoro, huku sehemu za mji huo zikikosa umeme na maji.

Katika taarifa yao ya pamoja, wakuu wa mashirika ya kibinadamu walizitaka pande zinazopigana kuwalinda raia, kuwezesha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu na kutangaza usitishaji mapigano kitaifa.

Akizungumzia pande mbili kuu zinazopigana nchini Sudan, SAF na RSF, Bwana Laerke amesema: “Tunataka majenerali hawa wapate njia ya kutatua tofauti zao si kwa vurugu zinazoua, kujeruhi, kubaka mamia ya maelfu ya watu Sudan, bali wafanye hivyo kwa njia nyingine”.

Wakiwa na wasiwasi kuhusu viwango vya chini vya ufadhili kwa ajili ya mgogoro huo, wahudumu wa misaada pia waliwataka wafadhili kutoa haraka ahadi walizotoa kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Kibinadamu kwa ajili ya Sudan na Majirani zake uliofanyika mjini Paris tarehe 15 Aprili.

Karibu miezi mitano tangu mwaka kuanza, ombi la misaada ya kibinadamu kwa Sudan lenye jumla ya dola bilioni 2.7 limefadhiliwa kwa asilimia 16 tu.