Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dola bilioni 4.1 zahitajika Sudan kwa ajili ya wakimbizi na masuala ya kibinadamu: OCHA/UNHCR

Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao katika eneo la Wakimbizi wa Ndani huko Darfur Magharibi kutokana na mapigano nchini Sudan.
© UNOCHA/Mohamed Khalil
Wanawake na watoto waliokimbia makazi yao katika eneo la Wakimbizi wa Ndani huko Darfur Magharibi kutokana na mapigano nchini Sudan.

Dola bilioni 4.1 zahitajika Sudan kwa ajili ya wakimbizi na masuala ya kibinadamu: OCHA/UNHCR

Msaada wa Kibinadamu

Ombi la pamoja limezinduliwa leo mjini Geneva Uswis na shirika la Umoja wa Mataifa la kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharira OCHA kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR ili kuwasaidia wakimbizi na masuala mingine ya kibinadamu nchini Sudan mwaka huu wa 2024.

Ombi hilo la dola bilioni 4.1 litashughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu ndani ya Sudan na kwa raia wa nchi hiyo waliokimbilia nchi za jirani.

Kwa mujibu wa mashirika hayo “Miezi kumi tangu mzozo huo kuzuka, nusu ya wakazi wa Sudan ambao ni takriban watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi. Zaidi ya watu milioni 1.5 wamekimbilia nje ya mipaka ya Sudan hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini.”

Kupanuka kwa wigo wa mapigano nchini Sudan ikiwa ni pamoja na katika jimbo ambalo ni kitovu cha chakula nchini humo, la Aj Jazirah kumezua mojawapo ya migogoro mikubwa zaidi ya watu kufiurushwa na ukosefu wa ulinzi duniani. 

Na hivyo njaa imekithiri, na karibu watu milioni 18 wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula.

Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.
© UNICEF/UNI492302/Mohamdeen
Watoto na familia wakikimbia kwa miguu kutoka Wad Madani, jimbo la Al Jazirah kufuatia mapigano ya hivi karibuni.

Mapigano makali yanaendelea 

Mashirika hayo ya OCHA na UNHCR yamesema mapigano makali yanaendelea kuharibu mifumo ya usambazaji maji na miundombinu mingine muhimu ya kiraia nchini Sudan, na karibu robo tatu ya vituo vya afya havina huduma katika majimbo yaliyoathiriwa na migogoro. 

Magonjwa yakiwemo kipindupindu, surua na malaria yanaenea wakati ambapo theluthi mbili ya watu wanakosa huduma za afya. 

“Takriban watoto milioni 19 hawako shuleni. Ukiukaji wa haki za binadamu umeenea sana, huku kukiwa na ripoti zinazoendelea za unyanyasaji wa kijinsia.” yamesesisitiza mashirika hayo.

OCHA imesema inaratibu hatua ndani ya Sudan, huku mpango wa mahitaji ya kibinadamu na hatua kwa mwaka huu ukitoa wito wa dola bilioni 2.7 kufikia watu milioni 14.7. 

UNHCR kwa upande wake imesema inaratibu mpango wa Kikanda wa kukabiliana na changamoto ya wakimbizi, ambao unaomba dola bilioni 1.4 na unalenga karibu watu milioni 2.7 katika nchi tano jirani na Sudan.

Kwa pamoja, mipango yote miwili inalenga kusaidia watu milioni 17.4 nchini Sudan na katika Kanda.

Vita imewapora Wasudan karibu kila kitu

Mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa OCHA, Martin Griffiths amesema "Miezi kumi ya vita imewapora watu wa Sudan karibu kila kitu kuanzia usalama wao, nyumba zao na maisha yao. Ukarimu wa wafadhili unatusaidia kutoa chakula na lishe, makazi, maji safi, na elimu kwa watoto, na kupambana na janga hili la unyanyasaji wa kijinsia na matunzo kwa manusura, lakini ombi la mwaka jana ilifadhiliwa chini ya nusu.  Mwaka huu, ni lazima tufanye vizuri zaidi na kwa hisia ya uharaka zaidi."

Vita hivyo hadi sasa vimewalazimu zaidi ya watu milioni 1.5 kukimbilia nchi jirani ambazo tayari zilikuwa na rasilimali chache na zinazohifadhi idadi kubwa ya wakimbizi. 

Watu hao wanajumuisha wakimbizi na watu wanaolazimishwa kurejea katika nchi zao kabla ya wakati. 

OCHA inasema wengi wao wanafika katika maeneo ya mbali na magumu kufikia ambayo hayana huduma muhimu. 

Msaada kwa hatua za kibinadamu ni muhimu, lakini uwekezaji ili kuimarisha huduma za kitaifa na uthabiti wa jamii ni muhimu vile vile kusaidia Serikali zinazowakaribisha na kuwawezesha watu kuishi kwa heshima na utu.

Wakimbizi wa Sudan wamesimama nje ya nyumba yao katika kituo cha muda cha Kurmuk katika eneo la Benishangul-Gumuz kaskazini magharibi mwa Ethiopia.
© UNHCR/Tiksa Negeri
Wakimbizi wa Sudan wamesimama nje ya nyumba yao katika kituo cha muda cha Kurmuk katika eneo la Benishangul-Gumuz kaskazini magharibi mwa Ethiopia.

Jumuiya ya kimataifa lazima kuwashika mkono Wasudan

Naye Kamishina mkuu wa wakimbizi wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa UNHCR, Filippo Grandi amesema "Nimekutana na wakimbizi wa Sudan nchini Ethiopia na watu waliokimbia makazi yao ndani ya Sudan wamepoteza mengi sana. Na kila wakati tunasikia ujumbe sawa kutoka kwao ambao ni tunataka amani ili tuweze kurudi nyumbani, na tunahitaji usaidizi ili kujenga upya maisha yetu. “

Ameongeza kuwa watu hawa wanafanya kadiri wawezavyo ili kupata usaidizi wa msingi ambao jumuiya zinazowakaribisha na washirika wa kibinadamu wanaweza kuwapa. 

Hivyo Grandi amesema “Ninaiomba jumuiya ya kimataifa kuongeza uungaji mkono wao kwa watu wa Sudan. Wanahitaji sana msaada, na wanauhitaji sasa.”

Kuhusu msaada wa kibinadamu

Wahudumu wa misaada kutoka mashirika 167 ya kibinadamu walifikia watu milioni 7 nchini Sudan mwaka 2023, kwa msaada wa wafadhili wa kimataifa. Licha ya changamoto kubwa za ufikiaji, jumuiya ya kibinadamu iliwasilisha msaada wa kuokoa maisha katika maeneo yote ya migogoro nchini Sudan, na inaendelea kusaidia washirika wa ndani wa Sudan katika maeneo ambayo washirika wachache wa kimataifa wanaweza kufikia, ikiwa ni pamoja na Khartoum na Darfur. 

Ufikiaji wa kuvuka mpaka kutoka Chad umekuwa njia muhimu ya maisha, pamoja na njia nyingine zinazozingatiwa.

Mnamo 2023, washirika 64 waliunga mkono serikali mwenyeji katika kutoa msaada wa kibinadamu wa kuokoa maisha na ulinzi kwa zaidi ya watu milioni 1.5 katika nchi tano jirani za Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Chad, Misri, Ethiopia na Sudan Kusini. 

Mwaka huu 2024, Mpango wa Kukabiliana na Wakimbizi unalenga washirika 82 katika nchi tano kuendelea na msaada wa kuokoa maisha na kuunga mkono msaada wa kuwajengea watu milioni 2.7.