Bila usimamizi, Akili Mnemba itachochea mmomonyoko wa maadili
Bila usimamizi, Akili Mnemba itachochea mmomonyoko wa maadili
Mbobezi wa masuala ya elimu kutoka Malaysia Profesa Dkt. Selvaraj Oyyan amesema iwapo kasi ya sasa ya matumizi ya Akili Mnemba au AI haitapatiwa usimamizi wa kutosha, basi siku zijazo kati ya miaka 10 au 15 dunia itakuwa na watu wenye fikra na mtazamo mmoja kwani mashine zitakuwa zinafanya kila kitu.
Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa hivi karibuni kwenye jukwaa la 4 uwekezaji kwa wajasiriamali, WEIF4 lililoandaliwa kwa pamoja na shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda, UNIDO ofisi yake ya kuendeleza ugunduzi na teknelojia, ITPO nchini Bahrain, Profesa huyo wa teknolojia ya bailojia na vinasaba amesema jambo hilo linamtia hofu kubwa.
Amesema kwa miaka 15 iliyopita nimekuwa nikijikita sana kwenye usimamizi wa elimu. “Na kwa hivi karibuni nimekuwa nina wasiwasi sana kuhusu Akili Mnemba au AI. Bila shaka AI inaleta manufaa mengi viwandani na kwa wadau wengi na mengineyo.”
Akiwa mmoja wa wanajopo waliohudhuria jopo la kujadili mustakabali wa Akili Mnemba kwenye kusongesha malengo ya maendeleo endelevu, Profesa Pillay anakiri AI ina faida, lakini shaka na shuku yake yeye mtaalamu wa usimamizi wa elimu ni kwamba stadi za mahusiano na yaambatanayo na stadi hizo ambayo ni muhimu sana yakaendelezwa shuleni, lakini hivi sasa tunapoteza. Hayo tutayapoteza iwapo hatutakuwa na sera mahsusi ya kusimamia jambo hilo.
Nikamuuliza iwapo hofu ndio hiyo, na matumizi ya Akili Mnemba yanaongezeka hata kwenye kuandika imla shuleni, sasa nini kifanyike, na akasema “Kwa hiyo lazima kuweko na mizania kati ya Akili Mnemba na Maendeleo; na upande mwingine stadi za mahusiano ambazo tunahitaji kuziendeleza kwa wanafunzi. Iwapo hatutafanya hivyo, siku zijazo pengine miaka 10 au 15 ijayo tutakuwa na watu wenye mtazamo mmoja wa fikra, mashine zikitufanyia kila kitu. Je tuko tayari kwa hilo? Hilo ndio jambo nafuatilia sasa.”
Profesa akatamatisha na umuhimu wa usimamizi wa Akili Mnemba akisema kwamba hilo ni muhimu sana kwa kuwa dunia inahitaji kanuni na viwango sawa vya usimamizi.
“Sio tu kwa mabara bali dunia nzima. Ni muhimu tuzungumze lugha moja, tufanye kitu kimoja. La sivyo utakuwa na mataifa yanashindana. Usimamizi kwenye maadili, usalama wa data na kwenye utoaji wa maamuzi ili Akili Mnemba isijeathiri maadili ya kijamii. Kubwa zaidi maadili ya kibinadamu yasiharibiwe, hilo ni muhimu sana.”