Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nilikuwa na ujauzito wa miezi tisa nyumba yangu ilipopigwa bomu – Mkimbizi Sudan

Mkimbizi Sudan, Sara (akiwa na mtoto wake) ambaye alijifungua akiwa pekee yake bila usaidizi wa kitabibu.
IOM
Mkimbizi Sudan, Sara (akiwa na mtoto wake) ambaye alijifungua akiwa pekee yake bila usaidizi wa kitabibu.

Nilikuwa na ujauzito wa miezi tisa nyumba yangu ilipopigwa bomu – Mkimbizi Sudan

Amani na Usalama

Sara alikuwa na ujauzito wa miezi 9 wakati bomu lilipopiga nyumba yake na kumlazimu kukimbia na hatimaye kujifungua mtoto wake peke yake bila uangalizi wowote wa kitabibu. 

Familia nyingi nchini Sudan zimesambaratishwa na mzozo unaoendelea.

"Tulikuwa tunaishi Khartoum Mashariki. Hatukuwahi kuweka akilini mwetu wazo la kuondoka, lakini hali ilipoanza kuwa changamoto zaidi na mabomu yakawa mengi na hata bomu likaanguka kwenye nyumba yetu, hii ndiyo iliyotufanya tuamue kuondoka. Wakati huo huo, nilikuwa na ujauzito wa miezi 9 katika siku za mwisho za ujauzito wangu. Pia, jirani yetu aliuawa kwa bomu. Hili lilitutia hofu na kutulazimisha kuondoka.”

Mkimbizi Sudan, Sara ambaye alijifungua akiwa pekee yake bila usaidizi wa kitabibu.
IOM
Mkimbizi Sudan, Sara ambaye alijifungua akiwa pekee yake bila usaidizi wa kitabibu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) linakadiria kuwa mzozo huo wa Sudan umewaondoa takribani watu 58,000 kutoka El Fasher kaskazini mwa Darfur tangu Aprili Mosi mwaka huu. Watu wengi zaidi, wakiwemo watoto na wazee, hawawezi au wanazuiwa kuhamia maeneo salama zaidi. Sara akilengwa na machozi anaendelea kueleza.

“Nashukuru Mungu nilifika hapa na kujifungua kesho yake, nilikuwa nateseka. Baada ya kujifungua, bado ninateseka. Hatukuwa na chochote, tulilazimika kukopa pesa hata kuja hapa na sasa bado hatuwezi kurejesha."

Mamia ya maelfu ya raia wa Sudan huko El Fasher wanakabiliwa na hali mbaya zaidi ya kibinadamu. Maeneo mengi ya jiji yameachwa bila umeme wala maji. Idadi inayoongezeka watu ina ufikiaji mdogo wa mahitaji na huduma muhimu, pamoja na chakula na huduma za afya. Sarah anasema, "Nataka tu mahali salama. Ambapo naweza kuishi kwa raha.”