Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yataka msaada wa kuisaidia Chad kukabiliana na wakimbizi wanaowasili toka Sudan

Wakimbizi kutoka Sudan wanahamishwa kutoka kambi kwa kambi nchini Chad.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Wakimbizi kutoka Sudan wanahamishwa kutoka kambi kwa kambi nchini Chad.

UNHCR yataka msaada wa kuisaidia Chad kukabiliana na wakimbizi wanaowasili toka Sudan

Amani na Usalama

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kusaidia haraka wakimbizi nchini Chad, kwani idadi ya waliowasili imevuka 100,000.

Tangu kuanza kwa mzozo nchini Sudan tarehe 15 Aprili, takriban wakimbizi 100,000 wanaokimbia ghasia wamesaka hifadhi mashariki mwa Chad, hasa katika mikoa ya Ouaddaï, Sila, na Wadi Fira. Kwa mujibu wa taarifa ya UNHCR iliyotolewa leo mjini Ndjamena ripoti kutoka kwa timu za shirika hilo kwenye mpaka  mna Sudan zinaonyesha kuwa wimbi jipya la wanaowasili bado linaendelea.

Wengi wa wakimbizi hawa wapya wanatoka eneo la Darfur, nchini Sudan ambalo limeathiriwa sana na vurugu na kukabiliwa na ukosefu wa utulivu.

Inakadiriwa kuwa hadi watu 200,000 wanaweza kulazimika kukimbilia mashariki mwa Chad katika muda wa miezi mitatu ijayo.

UNHCR na wadau wanashirikiana na serikali

UNHCR na washirika wake wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na serikali ya Chad, kutoa msaada na kuratibu hatua za dharura kushughulikia mahitaji ya wakimbizi wapya waliowasili.

Laura Lo Castro, mwakilishi wa UNHCR nchini Chad amesema  "Tumekuwa tukifanya kazi usiku na mchana kutoa huduma za ulinzi, ikiwa ni pamoja na msaada maalum kwa waathirika wa ukatili na watoto walio katika hatari, kujenga visima vya maji, kuweka vyoo vya dharura, kuendesha kliniki zinazohamishika, kuandaa misafara ya kuhamisha wakimbizi, kuongeza uwezo wa kambi ili kuwahudumia wakimbizi wapya katika kambi zilizopo za wakimbizi, kujenga makazi ya familia na miundombinu ya jamii na tunaanza kujenga kambi mpya”.

Ameongeza kuwa “Kwa vile msimu wa mvua unakuja ndani ya wiki chache zijazo, tunahitaji vifaa vikubwa ili kuwahamisha wakimbizi kutoka maeneo ya mpakani kwa usalama na ulinzi wao. Tunahitaji kuanzisha mara moja kambi mpya na upanuzi wa kambi zilizopo na kuendelea kutoa usaidizi wa kibinadamu mpakani na mara wakimbizi wanapohamishwa. Kwa vile wenyeji pia wanaathiriwa pakubwa na hali nchini Sudan, baadhi ya usaidizi utahitaji kuongezwa kwa wale walio katika mazingira magumu zaidi miongoni mwa wenyeji.”

Shirika hilo limesisitiza kuwa ili kuendelea kuongeza juhudi za msaada wa kibinadamu na kuokoa Maisha wakati suluhu ya kudumu ya kuishi pamoja kwa amani ,usalama na utulivu ikisakwa shirika hilo linajitaji haraka fecha za ufadhili.

Makumi ya maelfu ya wakimbizi wamewasili Chad kutoka Sudan.
© UNHCR/Aristophane Ngargoune
Makumi ya maelfu ya wakimbizi wamewasili Chad kutoka Sudan.

Chad ilikuwa tayari mwenyeji wa wakimbizi

Kwa mujibu wa UNHCR kabla ya mzozo huu mpya kuanza Sudan, Chad tayari ilikuwa na wakimbizi takriban 588,770, wakiwemo Wasudan 409,819 waliokuwa wakikimbia vita huko Darfur kufikia Machi 2023.

Wakimbizi wengine ni 127,846 kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, Wanigeria 21,287 waliotoroka ghasia za Boko Haram katika kanda ya ziwa, 28,311 walioathiriwa na mivutano ya kijamii nchini Cameroon na wakimbizi 1,507 kutoka mataifa mengine.

Zaidi ya hao, inakadiriwa kuwa Wachadi 381,289 ni wakimbizi wa ndani, hasa katika mkoa wa Ziwa Chad.

Jamii zilizotawanywa zinaendelea kukabiliwa na ukosefu wa usalama nchini Chad na nchi jirani, unaochangiwa na uhaba wa chakula, utapiamlo, athari za mabadiliko ya tabianchi, na ukosefu wa fursa za kujikimu kimaisha.

Hali ya muda mrefu yawatu kutawanywa imeathiri huduma za msingi, maliasili, na mshikamano wa kijamii.

Licha ya mahitaji makubwa, hatua za misaada ya kibinadamu kwa majanga haya ya kutisha na magumu bado hazijafadhiliwa vya kutosha.

Wakimbizi walio katika mazingira magumu wanakosa msaada muhimu wa kuokoa maisha, na hivyo kutumbukia zaidi katika umaskini na njaa, na kuongeza uwezekano wao wa kukabiliwa na hatari za ulinzi.

Msaada wa kibinadamu ndio mkombozi kwa wengi

Lo Castro. Ameongeza kuwa "Kwa familia zilizotawanywaa na janga hili, msaada wa kibinadamu ni mwanga wao wa matumaini. Tunategemea huruma na ukarimu wa washirika wetu kukusanyika pamoja ili kuhakikisha utoaji wa ulinzi muhimu na msaada wa kuokoa maisha. Kwa pamoja, tunaweza kuokoa maisha na kurejesha utu kwa wale wanaouhitaji sana.”

UNHCR inahitaji dola milioni 214.1 kutoa ulinzi na msaada wa kuokoa maisha kwa watu waliotawanywa nchini Chad, ambazo zinajumuisha dola milioni 72.4 zinazohitajika haraka kwa ajili ya kukabiliana na dharura kwa wakimbizi wanaokimbia vita nchini Sudan.

Hata hivyo cha kusikitisha, ni kwamba mahitaji ya UNHCR kwa Chad kwa sasa yamefadhiliwa kwa asilimia 16 pekee.