Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ILO: Ukosefu wa ajira duniani kupungua kidogo mwaka 2024

wafanyakazi wa ujenzi wakiwa na nyundo
© Unsplash/Arron Choi
wafanyakazi wa ujenzi wakiwa na nyundo

ILO: Ukosefu wa ajira duniani kupungua kidogo mwaka 2024

Ukuaji wa Kiuchumi

Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Ajira ILO imeeleza kuwa makadirio mapya yanaonesha kuwa ukosefu wa ajira duniani utapungua kwa kiasi mwaka huu hata kama ukosefu wa usawa wa kijinsia katika soko la ajira utaendelea. 

Ripoti hiyo iliyopewa jina la Ajira ulimwenguni na mtazamano wa kijamii: Chapisho la mwezi Mei 2024 mbali na kueleza kuwa wanawake kutoka nchi za kipato cha chini ndio watakao athirika zaidi umetabiri kuwa kiwango cha ukosefu wa ajira duniani kwa mwaka 2024 kitakuwa asilimia 4.9, ikilinganishwa na mwaka 2023 ambapo ilikuwa asilimia 5.0. 

Mkurugenzi Mkuu wa ILO Gilbert F.Houngbo akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Geneva Uswisi ameeleza namna ripoti hiyo inavyoonesha changamoto sugu ya ajira duniani ambayo inapaswa kushughulikiwa. Amesema licha ya juhudi za kuondoa ukosefu wa usawa lakini soko la ajira linasalia kuwa eneo ambalo halina usawa hususan kwa wanawake. 

Houngbo amesema “ili kufikia ahueni endelevu ambayo manufaa yake yanashirikisha watu wote, lazima tuwe na sera shirikishi zinazozingatia ushirikishwaji na haki ya kijamii kwa wafanyakazi wote. Tulishindwa kufanya hivyi hatutafikia malengo yetu ya kuhakikisha kuna maendeleo imara na shirikishi.” 

Takwimu hizo mpya zinarekebisha kushuka kwa makadirio ya ajira yaliyotolewa hapo awali na ILO ya asilimia 5.2 kwa mwaka huu. Walakini, hali ya kushuka kwa ukosefu wa kazi inatarajiwa kupungua mwaka 2025, na ukosefu wa ajira ukisalia kwa asilimia 4.9, ripoti hiyo inasema.

Wanawake bado wako nyuma

Takwimu za kina kutoka katika ripoti hiyo zinaonesha kuwa wanawake, hasa katika nchi za kipato cha chini, wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa fursa. Pengo la ajira kwa wanawake katika nchi zenye kipato cha chini linafikia asilimia 22.8, ikilinganishwa na asilimia 15.3 kwa wanaume. 

Kwa upande wa nchi za kipato cha juu, kiwango cha utofauti, wanawake ni asilimia 9.7 kwa wanawake na wanaume ni asilimia 7.3.

Ripoti hiyo imeeleza kuwa takwimu hizo ni sawa na “tone katika Bahari”, kwani kwa kiasi kikubwa wanawake wengi zaidi kuliko wanaume wamejitenga kabisa na soko la ajira. Ripoti inagundua kuwa majukumu ya familia yanaweza kuelezea tofauti kubwa inayoonekana katika viwango vya ajira vya wanawake na wanaume. 

Ulimwenguni, asilimia 45.6 ya wanawake wenye umri wa kufanya kazi wameajiriwa kwa mwaka 2024, ikilinganishwa na asilimia 69.2 ya wanaume.

Hata pale wanapoajiriwa wanawake wanakuwa wanapata kipato cha chini ilinganishwa na wanaume hususan katika nchi zinazoendelea. “Wakati wanawake katika nchi zenye kipato cha juu wanapata senti sabini na tatu ikilinganishwa na dola inayopatikana kwa wanaume, takwimu hii inashuka hadi senti arobaini na nne tu katika nchi za kipato cha chini.”

Licha ya kupitishwa kwa Ajenda ya Maendeleo Endelevu mwaka 2015 ambayo itafikia kikomo mwaka 2030, maendeleo katika kupunguza umaskini yamepungua ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita. Idadi ya wafanyakazi katika ajira zisizo rasmi imeongezeka kutoka takriban bilioni 1.7 mwaka 2005 hadi bilioni 2.0 mwaka 2024. 

Ripoti hiyo imehitimisha kwa kueleza kuwa ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu, "mbinu za kina" za kupunguza umaskini na ukosefu wa usawa zinahitajika haraka.