Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sitisho endelevu la mapigano ndio jawabu la kudumu- WHO

Mgonjwa aliye na utapiamlo mkali na upungufu wa maji mwilini katika hospitali ya mashambani kusini mwa Gaza - Aprili 24, 2024
© WHO
Mgonjwa aliye na utapiamlo mkali na upungufu wa maji mwilini katika hospitali ya mashambani kusini mwa Gaza - Aprili 24, 2024

Sitisho endelevu la mapigano ndio jawabu la kudumu- WHO

Afya

Kutoka Geneva, Uswisi hii leo, Mwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO kwenye eneo linalokaliwa la Palestina, Dkt. Rik Peeperkorn amesema wanalaani vikali shambulio la jumapili dhidi ya wakimbizi wa ndani huko Al-Mawasi linalodaiwa kusababisha vifo vya watu takribani 45.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa Dkt. Peeperkorn amesema “shambulio hili dhidi ya wakimbizi linadhihirisha kuwa hakuna pahala salama Gaza,” amesema Dkt. Peeperkorn akimulika pia madhara ya mashambulizi ya hospitali dhidi ya huduma za afya kwa majeruhi.

Amesema ni vema kuwa wazi kuwa dawa muhimu zinahitaji kiwango maalumu cha joto na kadhalika. Hivyo wanahitaji kufuatilia dawa hizo kwa umakini kwani Tangu kufungwa kwa kivuko cha Rafah, wameweza kuingiza magari matatu tu Rafah ambayo yalipitia Kerem Shalom, na hayo ndio magari pekee. Kwa bahati mbayá bado tuna akiba lakini inamalizika haraka.

Afisa huyo wa WHO huko Gaza amerejelea wito wa kutaka kivuo cha Rafah kifunguliwe kwani kwa sasa kuna malori 60 ya WHO yakisubiri huko Al Arish tayari kuingia Gaza. “Kwa mara nyingine tena, ombi hili la kufungua kivuko cha Rafah sio tu kwa ajili ya kuingiza vifaa vya matibabu bali pia kwa shehena zote za misaada ya kiutu.”

Dkt. Peeperkorn amezungumzia pia majeruhi wenye majeraha ya kuungua akisema kuwa hawana pahala popote pa kupata matibabu na kibaya zaidi ni kwamba “tangu kufungwa kwa kivuko cha Rafah tarehe 6 mwezi Mei, hakuna mgonjwa yeyote aliyeweza kuhamishwa kutoka Gaza, jambo ambalo tayari lilikuwa changamoto tangu awali.”

Dkt. Rik Peeperkorn, Mkuu wa ofisi ya WHO huko Gaza na Ukingo wa Magharibi akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa  huko Geneva, Uswisi
UN News/Anton Uspensky
Dkt. Rik Peeperkorn, Mkuu wa ofisi ya WHO huko Gaza na Ukingo wa Magharibi akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi

Hospitali ya IMC na changamoto ya kuandaa miili ya waliouawa

Video kutoka hospitali ya mashinani ya  International Medical Corps, IMC, inayotibu majeruhi inaonesha baba aliyejeruhiwa akilia kwa machungu huku akisimulia wakati ambao watoto wake walikufa.

“Wakati kombora lilipopiga, nilikuwa nafikiria watoto wangu,” amesema Mohammad Al Ghouf. “ Niliwaahidi nitaenda dukani kununua vitu kadhaa na kisha niwakumbatie. Lakini kwa bahati mbaya niko hapa na wao wako pahala pengine,” amesema Bwana Al Ghouf kupitia video hiyo iliyosambazwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dhaura, OCHA.

Kutoka katika video hiyo hiyo ya OCHA iliyochukuliwa siku ya Jumatatu, Mkurugenzi wa tiba wa hosptali hiyo ya IMC amesimulia jukumu gumu wanalokabiliana nalo la kuandaa maiti kwa ajili ya mazishi.

Anasema, “niliona maiti ya baba mmoja ambaye kimsingi alikuwa amemshikilia mtoto wake mwenye umri wa pengine miaka mitatu. Walikuwa wameungua kama mkaa. Hatukuweza kuwatenganisha. Kwa hiyo tulilazimika kuwaweka miili yao wote wawili kwenye mfuko mmoja. Ilikuwa vigumu mno.”

Ni kwa mantiki hiyo Dkt. Peeperkorn amesisitiza umuhimu wa sitisho la mapigano kwani “kutakapokuweko na sitisho la mapigano na endelevu, na njia endelevu za kuingia Gaza zinazosimamiwa vizuri, pia mfumo wa kumaliza mzozo ambao unatoa usaidizi wa kutosha, mambo mengi zaidi yanawezekana.”