Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunahaha kuendelea na huduma za matibabu Gaza- Dkt. Al Mandhari

Dkt. Ahmed Al Mandhari, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Mediteranea Mashariki
Video ya UN News
Dkt. Ahmed Al Mandhari, Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Mediteranea Mashariki

Tunahaha kuendelea na huduma za matibabu Gaza- Dkt. Al Mandhari

Afya

Mkurugenzi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO) Kanda ya Mediterania ya Mashariki, Dk. Ahmed Al Mandhari, amesema jitihada za kuongeza upatikanaji wa vifaa muhimu vya matibabu kwa ajili ya Ukanda wa Gaza zinaendelea, na hatua zaidi zinachukuliwa kuhakikisha kuwa hospitali zinaweza kuendelea kutoa huduma muhimu kwa wagonjwa wakati huu ambapo mashambulizi dhidi ya hospitali na wahudumu wa afya yamedhoofisha utoaji huduma

Dk. Al Mandhari ametoa tathmini hiyo leo wakati akihojiwa kwa njia ya video na Idhaa ya Kiarabu ya Umoja wa Mataifa ambapo amesema tangu kuanza kwa mapigano siku 10 zilizopita, kumekuweko na mashambulizi 154 dhidi ya vituo vya afya na hospitali huko kaskazini mwa Gaza ambayo yamesababisha vifo vya wahudumu wa afya 15, na zaidi ya magari 70 ya wagonjwa yameshambuliwa.

“Kumekuweko na majeruhi miongoni mwa wagonjwa, na wahudumu wa afya,” amesema Dkt. Al Mandhari huku akiongeza kuwa hospitali nne kati ya 22 kwenye eneo hilo la Kaskazini mwa Gaza sasa hazifanyi kazi kabisa.

Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza. WHO yaonya kuwa hospitali katika Ukanda wa Gaza ziko katika hali mbaya.
WHO/Occupied Palestinian Territory
Hospitali ya Al-Shifa huko Gaza. WHO yaonya kuwa hospitali katika Ukanda wa Gaza ziko katika hali mbaya.

Alipoulizwa kuhusu hali ya upatikanaji wa vifaa vya matibabu, Mkurugenzi huyo wa WHO Kanda ya Mediteranea Mashariki amesema “kutokana na uhaba mkubwa wa vifaa, WHO inatambua kuwa hali ni mbaya sana,na baadhi ya vifaa havipatikani kabisa, vifaa vilivyosalia vinakaribia kuisha, pia upatikanaji wa maji safi katika hospitali na mafuta yanatosha kwa masaa machache hivyo unaleta wasiwasi, hii inamaanisha bila mafuta, hakutakuwa na umeme katika hospitali hizo.”

Kwa mujibu wa WHO kwa sasa hali ni mbaya kutokana na uhaba wa upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii na kiutu katika maeneo mbalimbali ya Gaza, baada ya Israeli kukata huduma ya umeme, maji huku ikiweka zuio la kutotaka kuingia kwa kwa kitu chochote katika ukanda wa Gaza.

Hivyo Dkt. Al Mandhari amesema “WHO inazitaka pande zote zinazozozana kuzingatia sheria za kimataifa za kibinadamu, kuzingatia maadili na umhimu wa kulinda raia, umhimu wa kulinda vituo vya afya, na watu ambao wako katika maeneo haya”.

Hali hii inatokea wakati leo ni siku ya 4 tangu WHO ifikishe kwenye kivuko cha Rafah mpakani mwa Misri malori yenye shehena za meta za ujazo 78 za vifaa vya tiba na misaada muhimu ya kuokoa maisha, malori hayo yakisubiri kibali cha Israeli ili yaingie Gaza.