Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa amani wa UN unasalia kuwa ushirikiano wa kipekee wa kimataifa

Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya MINUSMA. (Maktaa)
MINUSMA/Harandane Dicko
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa wanaohudumu chini ya MINUSMA. (Maktaa)

Ulinzi wa amani wa UN unasalia kuwa ushirikiano wa kipekee wa kimataifa

Amani na Usalama

Leo ni siku ya kimataifa ya walindaamani wa Umoja wa Mataifa mwaka huu ikibeba maudhui “Kuwa tayari kwa ajili ya ujenzi wa mustakbali bora kwa pamoja”. Umoja wa Mataifa umesisitiza kuwa ulinzi wa amani unasialia kuwa ushirikiano wa kipekee  wa kimataifa.

Katika ujumbe wake kwa siku hii Antonio Guterres amesema "Leo tunawaenzi walinda amani zaidi ya 76,000 wa Umoja wa Mataifa ambao wanadumisha lengo bora zaidi la ubinadamu, amani. Siku baada ya siku, wakihatarisha Maisha yao, wanawake na wanaume hawa wanafanya kazi kwa ujasiri katika baadhi ya maeneo hatari na yasiyo na utulivu duniani ili kulinda raia, kudumisha haki za binadamu, kumsaidia masuala ya uchaguzi na kuimarisha taasisi. Zaidi ya walinda amani 4,300 wamelipa gharama ya Maisha yao wakati wakihudumu chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa. Hatutawasahau kamwe.”

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa maudhui ya siku ya mwaka huu yanaashiria kwamba wakati ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa umethibitika kuwa sehemu ya suluhu kwa zaidi ya miaka 75 ukizisaidia nchi mwenyeji kuvuka mapito kutoka kwenye migogoro hadi amani muhtasari wa Sera wa Katibu Mkuu wa Ajenda mpya ya amani unaweka njia ya operesheni za kimataifa za amani na usalama mbele ili kusalia kuwa zana zinazofaa kushughulikia vita na migogoro ijayo.

Naye mkuu wa operesheni za Umoja wa Mataifa za ulinzi wa amani Jean-Pierre Lacroix,akiongeza sauti yake katika siku hii amesema "Ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa unasalia kuwa ushirikiano wa kipekee wa kimataifa, huku walinda amani kutoka zaidi ya nchi 120 wakifanya mabadiliko yenye tija kila siku kwa mamilioni ya watu katika baadhi ya maeneo magumu zaidi duniani. Tunapokabiliana na changamoto za kesho, ulinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa unaendelea kubadilika, na kuhimiza ushirikiano kuwa mahiri, msikivu na unaofaa kwa madhumuni yaliyokusudiwa, kukuza utulivu, kulinda walio hatarini na kusaidia kujenga amani ya kudumu."

Siku ya Kimataifa ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa inaadhimishwa kila mwaka Mei 29 na ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2002 ili kuwaenzi wanaume na wanawake wote katika operesheni za ulinzi wa amani na kuenzi kumbukumbu ya wale wote waliopoteza Maisha yao kwa lengo la kuleta amani.