Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Majaribio ya nyuklia yameathiri binadamu na mazingira:Guterres 

Jaribio la nyuklia lililofanywa na Marekani katika eneo la Enewetak Atoll, Marshall Islands, 1 Novemba 1952.
US Government
Jaribio la nyuklia lililofanywa na Marekani katika eneo la Enewetak Atoll, Marshall Islands, 1 Novemba 1952.

Majaribio ya nyuklia yameathiri binadamu na mazingira:Guterres 

Amani na Usalama

Majaribio ya nyuklia yamesababisha mateso makubwa na athari kwa binadamu na uharibifu wa mazingira.  

Huku mengi yakiwa na athari mbaya kwa afya ya watu wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake kwa ajili ya siku ya kimataifa ya kupinga majaribiom ya nyuklia. 

Guterres ameongeza kuwa watu wengi walilazimika kuhamishwa kutoka katika ardhi za mababu zao, wakivuruga maisha yao na na uwezo wao wa kujikimu kimaisha huku mfumo mzima wa mazingira na mifumo ya ikolojia ikiharibiwa, ambayo itachukua miongo, ikiwa sio karne nyingi kuweza kupona na kurejea katika hali yake. 

Leo pia inaadhimishwa miaka 30 tangu kufungwa kwa eneo la majaribio ya nyuklia la Semipalatinsk huko Kazakhstan, kituo kikubwa zaidi cha majaribio ya nyuklia katika nchi za muungano wa Kisovyeti.  

Kufungwa kwa kituo hicho, ambako majaribio zaidi ya 450 ya nyuklia yalifanyika, iliashiria kumalizika kwa enzi ya kuzalisha nyuklia bila kizuizi.  

Muda mfupi baada ya kufungwa kwa eneo hilo, nchi zilianza kujadili mkataba kamili wa kupinga majaribio ya nyuklia , CTBT, ambao ulipitishwa miaka mitano baadaye. 

Jaribio la nyuklia lililofanywa katika kisiwa cha Ufaransa cha Polynesia mwaka 1971
CTBTO
Jaribio la nyuklia lililofanywa katika kisiwa cha Ufaransa cha Polynesia mwaka 1971

Miongo mitatu baada ya kufungwa Semipalatinsk 

Katibu Mkuu amesema “katika miongo mitatu kufuatia kufungwa kwa tkituo cha Semipalatinsk, tumeshuhudia maendeleo ya hatua kwa hatu ya utaratibu wa dhidi ya majaribio ya nyuklia.” 

CTBT inapiga marufuku majaribio yote ya mlipuko wa silaha za nyuklia za mahali popote, na nchi yoyote, na kusitisha mbio za mashindano ya silaha za nyuklia na kutoa kizuizi chenye nguvu kwa utengenezaji wa silaha mpya za nyuklia.  

Hata hivyo Guterres amesema, uwezo kamili wa CTBT haujatekelezwa, kwani mkataba huo haujaanza kutumika licha ya kukubalika karibu na mataifa yote ulimwenguni. 

“Ninasisitiza tena nchi hizo ambazo bado hazijaridhia mkataba huo kufanya hivyo bila kuchelewa. Mataifa manane ambayo kuridhia kwake kwa mkataba huu ni muhimu ili uanze kutumika yana jukumu maalum. Wakati huo huo, Mataifa yote yanapaswa kudumisha au kutekeleza masharti kuhusu milipuko ya nyuklia.” 

Katibu Mkuu amehitimisha ujumbem wake kwa kusema kuwa siku ya kimataifa ya Kupambana na majaribio ya nyuklia ambayo huadhimishwa kila mwaka Agosti 29 ni fursa ya kuthibitisha ahadi yetu ya kukataza majaribio yote ya nyuklia, kwa mtu yeyote, mahali popote. Hakuna kisingizio cha kuchelewesha kufikia lengo hili.