Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ulinzi wa amani uwe na mkakati wa kudhibiti habari potofu na za uongo

Jenerali Birame Diop, Mshauri wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kijeshi
UN Video
Jenerali Birame Diop, Mshauri wa Umoja wa Mataifa wa Masuala ya Kijeshi

Ulinzi wa amani uwe na mkakati wa kudhibiti habari potofu na za uongo

Amani na Usalama

Mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya kijeshi, Jenerali Birame Diop amesema kadri binadamu wataendelea kuweko duniani mizozo na majanga vitaendelea kuweko na hivyo kinachohitajika ni mfumo wa kupunguza uweko na utatuzi wa majanga hayo.

Akihojiwa na Idhaa ya Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha siku ya ulinzi wa amani duniani, Jenerali Diop ambaye anatamatisha jukumu lake anasema angalau kwa sasa kuna jawabu la ulinzi wa amani ambalo licha ya changamoto zake linaleta nuru.

Jenerali Diop amesema ulinzi wa amani umethibitisha kuwa unaweza kutatua baadhi ya mizozo akitolea mfano “Timor-Letse, Côte d'Ivoire, Sierra Leone na  Liberia, ambako ulinzi wa amani umesaidia kurejesha amani na utulivu. Na sasa nchi hizi hata zinashiriki kwenye ulinzi wa amani.”

 Côte d'Ivoire, ilikuwa imetuma walinda amani kuhudumu kwenye ujumbe wa kulinda amani nchini Mali, MINUSCMA, ujumbe uliofunga pazia rasmi mwaka jana wa 2023 baada ya kuhudumu tangu mwaka 2013.

Ingawa ulinzi wa amani unazaa matunda, kwa Jenerali Diop jambo muhimu ni kuzidi kuboresha huduma hiyo kwani itaendelea kuwa muhimu huku Umoja wa Mataifa ukihakikisha ujumbe wa ulinzi wa amani unapatiwa mamlaka na majukumu sahihi ili kukidhi mantiki ya uwepo wake. 

Na zaidi ya yote amesema “tunatakiwa pia leo hii kuambatanisha ujumbe wa ulinzi wa amani na mfumo wa kimkakati wa mawasiliano ili kuzuia habari potofu na habari za uongo zinazoharibu kila kitu tunachofanya. Ulinzi wa amani hautafanikiwa iwapo nchi mwenyeji haiungi mkono ujumbe wa ulinzi wa amani.”