Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya udugu duniani: Mkuu wa UN ahimiza mshikamano ulimwenguni

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ( Maktaba)
UN Photo/Evan Schneider
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ( Maktaba)

Siku ya udugu duniani: Mkuu wa UN ahimiza mshikamano ulimwenguni

Amani na Usalama

Leo ni siku ya udugu duniani, siku hii inaadhimisha kusherehekea kuheshimiana na mshikamano ambao unaunganisha watu duniani kuwa kama familia moja. 

Katika Ujumbe wake kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kwa sasa ulimwenguni madili hayo ya mshikamano na kuungana yamekuwa yakijaribiwa kutokana na kuibuka kwa migawanyiko, migogoro na ukosefu wa usawa huku ubaguzi ukikithiri. 

Guterres amesema ili kupambana na hali hiyo “Ni lazima tujumuike pamoja ili kulinda na kudumisha haki za binadamu, kupambana na kauli za chuki na misimamo mikali yenye jeuri, na kuwarudisha nyuma wale wanaofaidika kutokana na hofu.”

Amesema haya yanawezekana kwa kupata msukumo kutoka kwenye tamko la "Udugu kwa Amani ya Ulimwengu na Kuishi Pamoja" - lililoandikwa kwa pamoja na Mtakatifu Papa Francis na Mwadhama Imamu Mkuu wa Al-Azhar Sheikh Ahmed El Tayeb – likisihi kufanya kazi kuelekea ulimwengu ambao mazungumzo, huruma, na utu wa mwanadamu unatawala.

“Hebu tuthibitishe tena dhamira yetu ya kuziba migawanyiko, kukuza uelewano wa kidini na ushirikiano kati ya watu wa tamaduni na imani zote. Kwa pamoja, tutengeneze njia kuelekea ulimwengu wenye amani zaidi, wa haki na wenye usawa kwa wote.” Alihitimisha Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake.