Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaishika mkono Papua New Guinea kufuatia maporomoko ya ardhi

Wahudumu wa uokozi wakiwa katika eneo lililoathirika na maporomoko ya ardhi Kaskazini mwa Papua New Guinea
UNDP
Wahudumu wa uokozi wakiwa katika eneo lililoathirika na maporomoko ya ardhi Kaskazini mwa Papua New Guinea

UN yaishika mkono Papua New Guinea kufuatia maporomoko ya ardhi

Tabianchi na mazingira

Umoja wa Mataifa unaendelea kuisaidia mamlaka nchini Papua New Guinea (PNG) kwa juhudi za utafutaji na uokoaji siku nne baada ya maporomoko makubwa ya ardhi katika jimbo la Enga, ambapo takriban watu 2,000 wanahofiwa kufariki dunia na kuwafikia manusura bado ni changamoto.

Miili sita imepatikana hadi sasa na idadi inatarajiwa kuongezeka, imesema leo Timu ya Umoja wa Mataifa nchini humo UNCT.

Jumla ya watu walioathirika, ikiwa ni pamoja na wale wanaohitaji uwezekano wa kuhamishwa na kuhamishiwa mahali kwingine, inakadiriwa kuwa watu 7,849, au kaya 1,427, huku wengi wao wakiwa na chini ya umri wa miaka 16.

Na pia jumla ya miundombinu 150 inakadiriwa kuzikwa na maporomoko hayo.

Kubomoka kwa daraja

Ingawa usalama katika jimbo la mbali la kaskazini umeathiriwa na mapigano ya kikabila, utoaji wa misaada kwa sasa hautishiwi moja kwa moja na machafuko hayo.

UNCT imeripoti, hata hivyo, kwamba daraja katika mojawapo ya njia kuu katika eneo la milima liliporomoka Jumanne asubuhi, na hivyo kutatiza ufikiaji na kuleta changamoto ya mawasiliano kati ya Enga na maeneo mengine ya eneo hilo.

Njia mbadala ya kwenda Enga ni kupitia barabara kuu nyingine ambayo inaweza kuchukua hadi saa tatu zaidi, hivyo Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo linatathimini suluhu za kukarabati daraja haraka iwezekanavyo.

Taswira ya barabara kuu ya Porgera huko Papua New Guinea, baada ya maporomoko ya udongo kupiga jimbo la Enga, kaskazini mwa nchi hiyo iliyoko bahari ya pasifiki
IOM/ Mohamud Omer
Taswira ya barabara kuu ya Porgera huko Papua New Guinea, baada ya maporomoko ya udongo kupiga jimbo la Enga, kaskazini mwa nchi hiyo iliyoko bahari ya pasifiki

Hofu ya maafa zaidi

Juhudi za uokoaji pia zinatatizwa na hofu kwamba ardhi iliyojaa maji inaweza kuporomoka tena, na huku mvua kubwa ikiendelea kunyesha, kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM.

"Hatutaki maafa zaidi juu ya ya sasa," amesema leo Itayi Viriri, msemaji wa IOM kanda ya Asia na Pasifiki, akizungumza kwa njia ya Zoom kutoka Bangkok.

Maporomoko ya ardhi yalitokea saa tisa alfajiri siku ya Ijumaa, saa za Papua New Guinea, "wakati watu wengi walikuwa wamelala", amewaambia waandishi wa habari huko Geneva, yakizika nyumba, miundombinu na mashamba chini ya hadi mita nane za udongo na uchafu.

Ameongeza kuwa "Watu wengi ambao wameathiriwa na maporomoko haya kwa kweli walihamia eneo hili baada ya kukimbia migogoro ya kikabila katika maeneo mengine ya jimbo la Enga. Kwa hivyo hawa ni watu ambao tayari wamehama ambao sasa wanalazimika kuhama tena na kuhamia maeneo mengine”.

Maporomoko ya udongo ya Mei 25 Papua New Guinea yamesababisha maafa makubwa
UNDP
Maporomoko ya udongo ya Mei 25 Papua New Guinea yamesababisha maafa makubwa

Changamoto ya maji ya kunywa

IOM imeonya kwamba kutokana na miili mingi bado kuopolewa kutoka chini ya vifusi, wasiwasi unazuka iwapo maji ya chini ya ardhi yanayotiririka chini ya mlima yatachafua vyanzo vya maji ya kunywa.

“Kinachohitajika sasa, ni wazi, kwamba ni upatikanaji wa maji safi, maji mengi ambayo kwa kawaida jamii ingeyapata tayari yapo chini ya vifusi,” amesema Bwana. Viriri.

Ameongeza kuwa "Kwa hivyo, ikiwa ni pamoja na chakula, bila shaka, mavazi, vifaa vya malazi, vyombo vya jikoni, chochote ambacho kitajaribu na kupunguza ugumu ambao watu wanakabili hivi sasa kitasaidia."

Ombi la msaada

Kituo cha Kitaifa cha Maafa kimemwandikia Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Papua New Guinea kuomba msaada wa kimataifa. 

Washirika wote pia wanasisitizwa kushirikiana na kuratibu misaada kupitia Kituo hicho na vyombo vya usimamizi wa maafa vya mkoa.

Mahitaji ya haraka ni pamoja na maji safi, chakula, nguo, vifaa vya kujihifadhi, vyombo vya jikoni, dawa na vifaa vya usafi na msaada wa kisaikolojia na kijamii. Mamlaka za mkoa pia zimeiomba jumuiya ya kimataifa kupeleka mara moja wahandisi wa kijiografia ili kufanya tathmini ya hatari ya kijiografia.

Umoja wa Mataifa umekuwa ukisaidia mamlaka ya nchi hiyo tangu kuanza kwa maafa, ikiwa ni pamoja na katika shughuli za utafutaji na kurejeshaji, uanzishaji wa vituo vya dharura, na tathmini ya mahitaji ya awali na ya haraka.

Mamia ya watu wamezikwa kwenye maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Yambali Papua New Guinea
SIPA Benjamin
Mamia ya watu wamezikwa kwenye maporomoko ya ardhi katika kijiji cha Yambali Papua New Guinea

Tayari UN iko hapo

Wafanyakazi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM na la Mpango wa Maendeleo UNDP wako kazini, pamoja na Mshauri wa Uratibu wa Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa pia unaratibu juhudi za kukabiliana na wabia wote, katika ngazi ya kitaifa na mikoa, pamoja na kusaidia serikali katika kushughulikia mahitaji ya haraka.

IOM, UNDP, Shirika la Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto UNICEF, Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu na afyua ya Uzazi UNFPA na shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya wanawake UN Women watatoa misaada ya kawaida ya kibinadamu na usaidizi wa kisaikolojia, kwa uratibu na timu ya eneo hilo ya  kukabiliana na dharura.

UNICEF inaimarisha hatua zake za dharura na hadi sasa imesambaza kiasi kikubwa cha vifaa vya usafi na hedhi, vinavyojumuisha ndoo, madumu ya maji na sabuni pamoja na taulo za kike zinazoweza kutumika tena, vitambaa na vitu vingine ambavyo vilikuwa vimetangulizwa na Mamlaka ya Afya ya Mkoa.

"Tunafanya kazi kwa karibu na mamlaka ya Papua New Guinea na mashirika ya jamii ili kutoa msaada muhimu kwa manusura wa janga hili baya," amesema Mwakilishi wa UNICEF Angela Kearney.

Ameongeza kuwa "Sasa ni wazi kwamba zaidi ya asilimia 40 ya walioathiriwa ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 16 ambao wamehuzunishwa sana na kupoteza familia zao, nyumba, na riziki."