Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Muhtasari wa Habari: Papua New Guinea, Gaza, na SIDS

Mamia ya watu wamefukiwa kutokana na maporomoko ya udongo kwenye kijiji cha Yambali jimbo la Enga nchini Papua New Guinea tarehe 24 Mei 2024
IOM/ Mohamud Omer
Mamia ya watu wamefukiwa kutokana na maporomoko ya udongo kwenye kijiji cha Yambali jimbo la Enga nchini Papua New Guinea tarehe 24 Mei 2024

Muhtasari wa Habari: Papua New Guinea, Gaza, na SIDS

Tabianchi na mazingira

Muhtasari wa habari zetu hii leo unaangazia maporomoko ya udongo Papua New Guinea, Hali mbaya inayoendelea Gaza na mkutano wa nne wa SIDS

Nchini Papua New Guinea Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia mamlaka za mitaa katika jitihada za utafutaji na uokozi zinazoongozwa na Jeshi la Ulinzi la nchi hiyo kufuatia uharibifu mkubwa uliosababishwa na maporomoko ya ardhi majuzi tarehe 24 Mei katika jimbo la Enga. Kulingana na Kituo cha Kitaifa cha Maafa nchini humo, zaidi ya watu 2,000 wamefukiwa chini ya vifusi baada ya maporomoko hayo makubwa, yaliyosababishwa na mvua kubwa na kusababisha moja ya maafa mabaya zaidi katika historia ya hivi karibuni ya nchi hiyo.

Timu za UNRWA zinaendelea kutoa huduma za matibabu katika vituo vinane vya afya na makazi ya muda huko Gaza.
© UNRWA
Timu za UNRWA zinaendelea kutoa huduma za matibabu katika vituo vinane vya afya na makazi ya muda huko Gaza.

Wakimbizi wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na dharura ya kiafya isiyokuwa na mfano wake iliyosababishwa na vita mbaya zaidi katika historia ya Gaza, kwa mjibu wa ripoti ya UNRWA, iliyotolewa leo.  Katika maeneo Matano ya operesheni za UNRWA Jordan, Lebanon, Ukingo wa Magharibi, ikiwa ni pamoja na Jerusalem Mashariki, Gaza, na Syria, zaidi ya wagonjwa milioni mbili wanategemea huduma za afya za Shirika hilo. Katika taarifa nyingine OCHA imeeleza leo kwamba ubomoaji majengo umeripotiwa asubuhi ya leo huko Ein ad Duyuk katika eneo la Tahta na Silwan, na pia huko Al 'Isawiya na Kambi ya Aqabat Jaber katika Ukingo wa Magharibi, kwenye eneo Palestina linalokaliwa kimabavu.

Mtazamo wa St. John mji mkuu wa Antigua and Barbuda kunakofanyoika mkutano wa SIDS4
© UNICEF/Roger LeMoyne
Mtazamo wa St. John mji mkuu wa Antigua and Barbuda kunakofanyoika mkutano wa SIDS4

Na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo Mei 28 ameuambia Mkutano wa nne wa Kimataifa wa Nchi za Visiwa Vidogo Zinazoendelea (SIDS4) unaofanyika huko St John's, Antigua na Barbuda kwamba ulimwengu unahitaji kuchukua hatua katika nyanja tatu ili kusaidia vyema na kuhamasisha ufadhili kwa Nchi za Visiwa Vidogo Zinazoendelea (SIDS) ili kukidhi mahitaji na matarajio ya nchi hizo. Guterres amezitaja hatua hizo kwamba; kwanza, ni lazima kupunguza mzigo wa madeni. Pili, lazima kubadilisha utaratibu wa ukopeshaji. Na tatu, kunahitajika ushirikishwaji mkubwa katika taasisi za fedha za kimataifa.