Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

ICC yaomba hati za kukamatwa viongozi wa Hamas na Netanyahu wa Israel

Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Loey Felipe
Karim Khan, Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), akitoa maelezo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

ICC yaomba hati za kukamatwa viongozi wa Hamas na Netanyahu wa Israel

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, Karim Khan ametangaza leo Mei 20 maombi ya hati za kukamatwa viongozi wa Hamas na Israel kwa madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu katika eneo la Gaza. 

Ni Karim Khan, Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mapema leo alipotangaza kwamba anawasilisha maombi ya hati za kukamatwa viongozi wa Hamas na wa Israel kwa majaji wa mahakama hiyo ambao ndio watakaotoa uamuzi wa kutolewa kibali cha kukamatwa.

Bwana Khan amesema kuna sababu za msingi za kuamini kwamba Yahya Sinwar wa Hamas, Mohammed Diab Ibrahim Al-Masri (Deif) na Ismail Haniyeh "wanawajibikia kijinai" kwa mauaji, kuangamiza na kuchukua watu mateka miongoni mwa uhalifu mwingine mwingi tangu mzozo wa Gaza ulipozuka kufuatia mashambulizi yaliyoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba mwaka jana 2023.

“Pia kuna misingi ya kuridhisha ya kuamini kwamba Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant, Waziri wa Ulinzi wa Israel, wanahusika na uhalifu mwingine na uhalifu dhidi ya ubinadamu uliofanywa katika eneo la Palestina” Amesema Mwendesha Mashitaka wa ICC.

Ametaja miongoni mwa vitendo vya uhalifu wa kivita vilivyotekelezwa kuwa ni pamoja na kutumia njaa dhidi ya raia kama mbinu ya vita na pia kuelekeza kwa makusudi mashambulizi dhidi ya raia.

Ingawa ICC si shirika la Umoja wa Mataifa, ina makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Mataifa. Na kunapotokea suala ambalo haliko ndani ya mamlaka ya Mahakama, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linaweza kulipeleka suala hilo kwa ICC, na kuipa mamlaka ya kulishughulikia.

Tutaendelea kukupa taarifa kwa kina kuhusu hatua hii ya ICC ingawa pia kwa sasa unaweza kujisomea zaidi katika wavuti wetu news.un.org/sw.