Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Catriona Laing aiaga Somaliland

Catriona Laing, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia na Mkuu wa Ujumbe wa Misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akihutubia katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya nchi hiyo. (Maktaba)
UN Photo/Eskinder Debebe
Catriona Laing, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia na Mkuu wa Ujumbe wa Misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia akihutubia katika kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali ya nchi hiyo. (Maktaba)

Catriona Laing aiaga Somaliland

Masuala ya UM

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia Catriona Laing ameendelea na ziara yake ya kuwaaga viongozi wa eneo hilo na sasa ametembelea Somaliland. 

Juzi Mei 12, Catriona Laing alikuwa  Dusmareb, mji mkuu wa jimbo la Galmudug katikati mwa Somalia ambako alipongeza juhudi za kupambana na ukeketaji. Kisha jana Mei 14 akatua Hargeisa mji mkuu wa Somaliland ambako  amekutana na uongozi na kujadili msaada wa Umoja wa Mataifa kwa maendeleo na juhudi za kibinadamu. Miongoni mwa aliokutana nao ni Rais Muse Bihi na wajumbe wa baraza lake la mawaziri na washauri.

"Tumekuwa na mjadala mzuri sana, na Rais amezungumza nami kuhusu mpango wa maendeleo, ambao unaweka maono yake ya muda mrefu ya kiuchumi kuhusu faida za 'uchumi wa buluu,' kuhusu madini, na kufikiria juu ya mabadiliko ya biashara ya mifugo kama tunajiandaa dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa watu wenye maisha ya kuhamahama. Tumezungumza kuhusu jukumu la Umoja wa Mataifa katika kuunga mkono kufanikisha dira ya kiuchumi na kazi nyingine zote tunazofanya kuhusu maendeleo ya kijamii, afya, elimu, kibinadamu na katika maeneo mengine.

Hali katika eneo la Laascaanood-Sool -ambako migogoro ilipamba moto mwaka jana, na kusababisha kupoteza maisha na maelfu ya watu kuyahama makazi yao pia ilijadiliwa kama anavyoeleza Bi Liang kwamba, "Kumekuwa na changamoto huko nyuma na sote tulifurahi kuona kwamba mambo yametulia, na Rais amenihakikishia kuwa ni lengo lake kwamba mambo yabaki shwari. Umoja wa Mataifa utafanya sehemu yake katika kutoa msaada wa kibinadamu na kutegua mabomu kwa manufaa ya watu katika eneo hilo.”

UN Hargeisa

Mwakilishi huyo Maalum wa Umoja wa Mataifa pia alichukua fursa hiyo kumtambulisha rasmi mkuu mpya wa ofisi ya Umoja wa Mataifa huko Hargeisa, Nikolai Rogosaroff, ambaye alichukua wadhifa wake Machi mwaka huu. Alielezea uwepo wake hapo kama ishara ya kujitolea kwa Umoja wa Mataifa kusaidia maendeleo ya ndani na juhudi za kibinadamu. Hivi sasa, zaidi ya mashirika kumi na mbili ya Umoja wa Mataifa, fedha na program yanafanya kazi Somaliland.

Bi. Laing atakamilisha kazi yake baadaye mwezi huu wa Mei.