Ukata ni changamoto ya kuwasaidia wakimbizi wa Somalia walioko Ethiopia: UNHCR
Ukata ni changamoto ya kuwasaidia wakimbizi wa Somalia walioko Ethiopia: UNHCR
Ethiopia inakabiliwa na dharura nyingi huku kukiwa na changamoto kubwa ya ufadhili duni limeonya leo shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na kuongeza kuwa huku kukiwa na watu wapya na wanaoendelea kutawanywa na kuteseka kutokana na ukame, nchi hiyo ya Afrika Mashariki inahaha kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya watu waliokimbia makazi yao nchini kote.
UNHCR inasema miezi miwili tangu ilipotoa ombi la msaada wa kuwasaidia maelfu ya wakimbizi wa Somalia walioingia Ethiopia mwezi Februari la dola milioni 116 hadi sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimia 2 pekee.
Wakati UNHCR na washirika wameweka kipaumbele kwa fedha zilizopo mbali na mahitaji mengine muhimu ili kuzindua hmpango wa usaidizi, huku watu wengi zaidi wakiwasili nchini kila siku, ukosefu wa fedha unaleta changamoto kubwa katika operesheni zao.
Watu wapatao 100,000 wameingia Ethiopia
Inakadiriwa kuwa takriban watu 100,000 wamekimbia migogoro na ghasia zinazoendelea makwao huko Laascaanood, katika eneo la Somaliland nchini Somalia.
Familia, wanawake, watoto, wazee na watu wenye ulemavu wamekimbia na kile tu walichoweza kubeba baada ya makombora na milipuko kuharibu nyumba zao na kuwalazimisha kutafuta usalama katika eneo la Doolo la Ethiopia.
Tangu kuanza kwa dharura hiyo UNHCR na washirika wakiunga mkono serikali ya Ethiopia wamekimbilia kutoa msaada wa kuokoa maisha.
Dawa, maji na vitu vingine vya msingi vimewasilishwa kwa zahanati za karibu na eneo hilo ili kuhakikisha kuwa zinaweza kusaidia sawa jamii zinazowapokea na wakimbizi.
Shirika hilo la wakimbizi limesema licha ya uhaba wa rasilimali za ndani, “jumuiya za wenyeji katika eneo lote zimefungua milango yao kwa karibu asilimia 80 ya watu wote waliokimbia makazi yao. “
Wakati wale ambao wanaweza wanakaa na familia za Ethiopia, wengine wanapata hifadhi chini ya miti, wakikabiliwa na hatari ya kushambuliwa na wanyama, wizi na unyanyasaji wa kijinsia. Wengi wanahitaji makazi, chakula na matibabu.
Zaidi ya wakimbizi 20,000 wamehamishwa
Zaidi ya wakimbizi 20,000 wa Somalia wamehamishwa na serikali ya Ethiopia na UNHCR kwa usaidizi wa washirika wengine kwenda kwenye eneo jipya la Mirqaan, ambako huduma zikiwemo usambazaji wa maji, makazi ya dharura na usafi wa mazingira zinatolewa.
Huduma ya wakimbizi na waliorejea (RRS) ya serikali ya Ethiopia wanaendesha usajili wa watu binafsi wa kibayometriki kwa usaidizi kutoka UNHCR.
Lakini kutokana na rasilimali chache, mapengo tayari yanaonekana na UNHCR inahofia kwamba bila msaada wa haraka matokeo kwa wakimbizi na wenyeji wao yatakuwa mabaya.
"Tumefika pomoni mwa mgogoro wa mateso makubwa ya kibinadamu ikiwa tutashindwa kuleta msaada unaohitajika katika eneo hili," alisema Mamadou Dian Balde, mwakilishi wa UNHCR nchini Ethiopia.
Ameongeza kuwa "Rasilimali hazitoshi kutoa misaada ya kibinadamu na kuhakikisha suluhu kwa watu hao."
Kupunguzwa kwa huduma
UNHCR imesema katika makazi mapya, usambazaji wa maji umepunguzwa sana na gharama ya mafuta ya malori, na makadirio kuwa rasilimali za sasa zitadumu kwa miezi minne pekee.
“Hata sasa, wakimbizi wanaweza tu kupokea lita 10 za maji kwa kila mtu kwa siku, chini ya kiwango cha lita15 zinazohitajika. Ni asilimia 30 tu ya makao yanayohitajika ndiyo yaliyopo, na kuziacha baadhi ya familia katika vituo vyenye msongamano mkubwa au kulala mahali pa wazi katika jumuiya za wenyeji.”
Msaada kwa wakimbizi wanaokaa katika jumuiya za wenyeji pia umepunguzwa katika miji ya Docmo, Hegalle, Mirqaan na Goob, ambako Waethiopia tayari wanakabiliwa na changamoto kutokana na ukame mkali na ukosefu wa huduma za msingi.
UNHCR na washirika wake hawajaweza kuvisaidia mara kwa mara vituo vya matibabu kushughulikia mahitaji yote haswa kwa wale wanaohitaji huduma ya magonjwa sugu na magonjwa mengine, akina mama wajawazito, pamoja na manusura wa ubakaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia.
Msaada wa makazi na mahitaji mengine muhimu ni mdogo sana kwa mujibu wa shirika hilo la wakimbizi na, tathmini za mahitaji yanayosubiriwa, yanaweza kupatikana kwa watu wachache sana.
Pia shirika hilo limesema usambazaji wa chakula utakuwa mdogo kwa maeneo fulani kwa sababu ya uhaba wa mafuta, na elimu haitapatikana kwa watoto wengi kutokana na uwezo mdogo wa madarasa ambapo walimu tayari wamezidiwa uwezo.
Athari kwa jamii za wenyeji
UNHCR imesema inahofia jinsi ukosefu wa ufadhili unavyoathiri pia jumuiya zenye ukarimu za wenyeji ambazo zimewapokea wakimbizi na kugawana nao rasilimali zao.
Imeongeza kuwa kuongezeka kwa uhaba wa vitu na huduma muhimu kunaweza kuwa na matokeo ya janga katika kuishi kwa amani na utulivu wa eneo hilo.
Kuongezeka kwa wakimbizi hivi karibuni kunamaanisha kuwa Ethiopia sasa inawahifadhi karibu wakimbizi milioni 1, lakini ukarimu wake haujalinganishwa na ufadhili wa kutosha.
"UNHCR inaendelea kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoa msaada kwa maelfu ya wakimbizi wa Somalia ambao tayari wamekumbwa na migogoro na ghasia. Hatuwezi kuwasahau na jumuiya wakarimu ambazo zimefungua milango yao,” ameongeza Dian Balde.