Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi huru na wa haki lazima ufanyike dhidi ya waliokufa Laas Canood: Turk

Geti la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis
UN Photo/Jean-Marc Ferré
Geti la kuingia kwenye makao makuu ya ofisi ya haki za binadamu OHCHR mjini Geneva Uswis

Uchunguzi huru na wa haki lazima ufanyike dhidi ya waliokufa Laas Canood: Turk

Amani na Usalama

Kutoka Geneva nchini Uswisi Kamisha Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa , Volker Turk ametoa wito kwa mamlaka ya Somalia kuhakikisha uchunguzi huru unafanyika bila upendeleo kufuatia mauaji yaliyotokea baada ya mapigano makali kuanzia tarehe 5 mwezi huu wa Februari nchini humo kati ya vikosi vya usalama na wanajamii wa ukoo wa Laas Canood.

Kwa mujibu wa Bwana Turk takriban watu 20 wameuawa na wengine 119 wakiwemo watoto wa jamii ya Laas Canood wamejeruhiwa.

Kamishna Turk amesema “Nina wasiwasi na ripoti kuwa mapigano bado yanaendelea leo na kuna madai ya kuwepo kwa majeruhi wapya.”

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa haki za binadamu “Mauaji haya ambayo yanawezekana kuwa ni ya kinyume cha sheria yamekuja mwezi mmoja baada ya takriban watu 20,000 kutawanywa na mapigano Laas Canood na yanaweza kuchangia watu kutawanywa zaidi na hivyo kuifanya hali ya kibinadamu ambayo tayari ilikuwa mbaya kuwa mbaya zaidi katika ukanda huo.”

Ametoa wito kwa mamlaka kuhakikisha uchunguzi unakuwa wa kuridhisha na kufuata haki ili kubaini wahusika na kuwawajibisha kwa njia ya usawa ikiwemo uharibifu wa nyumba ulioripotoiwa.

Laas Canood ipo katika mikoa ya Sool na Sanaag na majimbo yote mawili ya Somaliland na Puntland yanadai kuwa ni yake.