Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

DRC: Hali ya utulivu yarejea baada ya shambulio la wiki iliyopita

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
UN
Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

DRC: Hali ya utulivu yarejea baada ya shambulio la wiki iliyopita

Amani na Usalama

Hali ya usalama huko Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini,  mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC imeripotiwa kuwa tulivu, ikiwa ni takribani wiki moja baada ya mlipuko kwenye kambi ya wakimbizi uliosababisha vifo vya raia 18 na makumi kadhaa walijeruhiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, jijini New York, Marekani hii leo, Naibu Msemaji wa  Umoja wa Mataifa Farhan Haq amenukuu ofisi ya Umoja huo ya kuratibu misaada ya kibinadamu, OCHA ikisema wameweza kurejea  operesheni zao kwenye kambi hiyo ya wakimbizi siku iliyofuata.

“Sasa wanasambaza vyakula, maji na mahitaji mengine muhimu pamoja na huduma za matibabu,” amesema Bwana Haq.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO nalo limesema limepeleka tani 24 za dawa kwa watu waliojeruhiwa kwenye tukio hilo huko Goma.

Wakati huo huo, OCHA inasema ongezeko la mapigano huko Kivu Kaskazini limechochea wimbi jipya la ukimbizi.

Tangu mwanzoni mwa mwezi huu wa Mei, watu wapatao 80,000 wamesaka hifadhi kwenye mji wa Kalehe, ulioko jirani na jimbo la Kivu Kusini.

“Wimbi hilo jipya la wakimbizi limesababisha jimbo la Kivu Kusini kuzidiwa uwezo wa kutoa huduma, kwani tayari linahifadhi takribani wakimbizi milioni 2,” amesema Bwana Haq.

Kwa sasa kuna changamoto za kufikia mji wa Kalehe, kutokana na hali ya usalama na ukosefu wa miundombinu kama vile barabara za uhakika.

Amesema mazingira yake yanakwamisha usambazaji wa misaada ya kibinadamu, kwa wakimbizi wanaume, wanawake na watoto.

Wakati huo huo, imekumbushwa kuwa mpango wa usaidizi kwa DRC kwa mwaka huu wa 2024, ni dola bilioni 2.6, na hadi sasa limechangiwa dola milioni 443 sawa na asilimia 17.