Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Waandishi wa habari 44 waliuawa wakichunguza masuala ya mazingira

Mtoto akiwa juu ya lundo la mchanga ambao hutumiwa na wakazi wa eneo hili kujaribu kuzuia maji ya ziwa Albert yasiingie kwenye makazi yao.
UN/ John Kibego
Mtoto akiwa juu ya lundo la mchanga ambao hutumiwa na wakazi wa eneo hili kujaribu kuzuia maji ya ziwa Albert yasiingie kwenye makazi yao.

Waandishi wa habari 44 waliuawa wakichunguza masuala ya mazingira

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Hii leo ni siku ya kimataifa ya uhuru wa vyombo vya habari maudhui yakiwa Uandishi wa Habari wakati huu wa janga la mazingira ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kwa kushirikiana na shirikisho la waandishi wa habari duniani, IFJ wametoa ripoti yao ikionesha kuwa ni katika kipindi cha miaka 15 iliyopita waandishi wa habari 44 waliuawa wakiwa wanachunguza masuala ya mazingira. Kampeni ya siku hii ni kwamba kila habari kuhusu mazingira lazima isimuliwe hivyo waandishi wa habari walindwe.

Masuala hayo ni pamoja na jinsi sekta ya madini inavyochafua mazingira, migogoro ya ardhi hasa kwenye maeneo yenye maliasili na bila kusahau ukimbizi utokanao na uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Kipindi hicho cha miaka 15 ni kuanzia mwaka 2009 hadi 2023.

Guilherme Canela, Mkuu wa Kitengo cha Uhuru wa Vyombo vya Habari na Usalama wa Waandishi wa Habari, UNESCO akizungumza na Idhaa ya Umoja wa Mataifa amesema, tumebaini kuwa waandishi wa habari 44 waliuawa katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kwa sababu walikuwa wanaandika habari kuhusu mazingira.

Akinukuu ripoti hiyo mpya itokanayo na utafiti utafiti uliohusisha waandishi wa habari 905 kutoka nchi 129 zikiwemo za bara la Afrika, Bwana Canela anasema katika hao 44 waliouawa, ni kesi tano tu ndio wahusika walipatikana na hatia na kuhukumiwa.

Waandishi wa habari walishambuliwa kimwili na mtandaoni

Asilimia 70 ya waandishi wa habari waliohojiwa walikumbwa na ghasia wakichunguza masuala ya mazingira kama vile uchafuzi utokanao na uchimbaji madini na migogoro ya ardhi. Asilimia 41 kati yao hao walipata mashambulio ya mwilini wengi wao wakiwa wanaume, ilhali asilimia 60 walishambuliwa mtandaoni, walengwa wengi wakiwa ni wanawake. Bara la Afrika lilibeba theluthi mbili ya matukio ya mashambulizi ya mwilini.

Kama hiyo haitoshi, asilimia 25 walikabiliwa na kesi za madai kwa lengo la kuwanyamazisha. Bwana Canela akisema tuligundua pia matukio 749 katika nchi 89 ya mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari au vyombo vya habari kwa sababu tu ya kuripoti masuala ya mazingira. Na kwa bahati mbayá, watekelezaji wakuu wa vitendo hivi vya mashambulizi walikuwa ni watu wa serikali. Polisi, wanasiasa au watu wenye uhusiano na serikali kwa njia moja au nyingine.”

Waandishi wa habari walilengwa hata kwenye maandamano

Hata wakati wa maandamano waandishi wa habari walilengwa kwani ripoti hiyo ya kurasa 18 inasema katika kipindi hicho cha miaka 15 kuanzia mwaka 2019  hadi 2023, waandishi wa habari 194 walishambuliwa na matukio mengi ni barani Ulaya, Amerika Kaskazini, Amerika ya Kusini na Karibea.

Hivyo afisa huyu wa UNESCO akatoa wito wa shirika hilo ya kwamba “katika siku hii ya uhuru wa vyombo vya habari mwaka huu wa 2024 tunahitaji kusisitiza umuhimu wa ulinzi kwa waandishi wa habari wanaoripoti kuhusu masuala haya, kwa sababu kama si hivyo, tutabakiwa kuwa na maeneo ya ukimya, ambako huko wanajamii hawafahamu au hawajapatiwa taarifa kwa njia isiyoegemea upande wowote juu ya kile kinachoendelea kuhusiana na aina hizi za mivutano.”