Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yaeleza kusikitishwa na ripoti za mauaji nchini Burkina Faso

Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.
© Michele Cattani
Mwanajeshi kutoka Burkina Faso akiwa katika ulinzi kwenye mpaka wa Mali na Niger wakati wa operesheni ya kijeshi dhidi ya washukiwa wa ugaidi.

UN yaeleza kusikitishwa na ripoti za mauaji nchini Burkina Faso

Haki za binadamu

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu OHCHR imeeleza kusikitishwa sana na ripoti za mauaji ya idadi kubwa ya raia, ikiwa ni pamoja na watoto, katika vijiji kadhaa katika majimbo ya Yatenga na Soum yaliyoko kaskazini mwa nchi ya Burkina Faso katika miezi ya hivi karibuni katika mazingira ya jumla ya mapigano kati ya makundi yenye silaha na vikosi vya Burkinabè.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari kutoka Geneva Uswisi, msemaji wa OHCHR Marta Hurtado ameeleza kuwa “ingawa hatujaweza kuthibitisha taarifa hizi kwa uhuru kutokana na kushindwa kufikia eneo hilo, ni muhimu tuhuma za ukiukwaji mkubwa kama huu na dhuluma zinazofanywa na watendaji mbalimbali zifichuliwe na mamlaka za mpito zifanye uchunguzi wa kina, bila upendeleo na madhubuti.”

Chombo hicho cha ngazi ya juu cha Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu kimetaka wahusika wote kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria na haki za waathirika kulindwa ili watu waweze kuamini kuna utawala wa sheria na uwiano wa kijamii.

Bi. Hurtado pia amesema wanasikitishwa na kusimamishwa kwa muda kwa angalau vyombo viwili vya habari vya kimataifa kufuatia ripoti zao kuhusu baadhi ya matukio haya.

“Vikwazo vya uhuru wa vyombo vya habari na nafasi ya raia lazima viachwe mara moja. Uhuru wa kujieleza ikiwa ni pamoja na haki ya kupata habari ni muhimu katika jamii yoyote, na zaidi katika muktadha wa mpito nchini Burkina Faso.”