Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Njaa yaendelea kuitikisa dunia ikiwemo Sudan, Gaza na kwingineko: FAO

Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.
© UNRWA
Chakula kinagawiwa kwa Wapalestina waliokata tamaa.

Njaa yaendelea kuitikisa dunia ikiwemo Sudan, Gaza na kwingineko: FAO

Amani na Usalama

Ripoti mpya ya kimataifa iliyotolewa leo na shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO kuhusu mgogoro wa chakula duniani inasema karibu watu milioni 282 walio katika nchi 59 walikabiliwa na viwango vya juu vya njaa mwaka 2023 ambayo ni sawa na mtu 1 kati ya 5 na sasa wanahitaji hatua za haraka kuepushwa na baa la njaa.

Ripoti hiyo ya “Mgogoro wa kimataifa wa chakula” GRFC inasema kiwango cha watu wenye njaa duniani kiliongezeka kwa watu milioni 24 kutoka mwaka 2022 hadi 2023 na ni asilimia 21.5 ya watu waliofanyiwa tahimini  na hicho ni kiwango kikubwa sana ukilinganisha na ilivyokuwa kabla ya janga la coronavirus">COVID-19 limesema shirika la FAO likiongeza kuwa idadi ya walio na njaa duniani inaendelea kuongezeka.

Ripoti imetaja sababu kuu tatu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa janga la njaa duniani ambazo ni mosi migogoro na vita ambapo inasema inaathiri katika nchi 20 zilizo na jumla ya watu milioni 135 wanaokabiliwa na njaa zikiwemo Sudan, Yemen na Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Ripoti inasema wakati janga la COVID-19 lilipoikumba Dunia mwishoni mwa mwaka 2019 mtu 1 kati ya 6 katika nchi 55 duniani walikuwa wanakabiliwa na viwango vya kutia hofu vya kutokuwa na uhakika wa chakula ukilinganisha na mtu1 kati ya 5 mwaka mmoja baadaye.

Mariam Djimé Adam, mwenye umri wa miaka 33 mkimbizi kutoka Sudan akiwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Adre nchini Chad ambayo sasa inatumika kuhifadhi wakimbizi
© UNICEF/Mahamat
Mariam Djimé Adam, mwenye umri wa miaka 33 mkimbizi kutoka Sudan akiwa kwenye uwanja wa shule ya sekondari ya Adre nchini Chad ambayo sasa inatumika kuhifadhi wakimbizi

Sababu zinazochangia janga la njaa

Ripoti hiyo  imetaja sababu kuu tatu ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa janga la njaa duniani ambazo ni mosi migogoro na vita ambapo inasema inaathiri katika nchi 20 zilizo na jumla ya watu milioni 135 wanaokabiliwa na njaa zikiwemo Sudan, Yemen na Palestina katika Ukanda wa Gaza.

Mfano migogoro ya chakula iliongezeka kwa hali ya kutisha mwaka 2023, waandishi wa ripoti hiyo wamebainisha, wakitaja wasiwasi kuhusu hali ya Gaza na Sudan hii leo "ambapo watu wanakufa kwa njaa", amesema Gian Carlo Cirri, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, ofisi ya Geneva.

Baada ya karibu miezi saba ya mashambulizi ya Israel, “watu hawawezi kukidhi hata mahitaji ya msingi zaidi ya chakula. Wamemaliza mikakati yote na sasa kukabiliana na hali hiyo, wanalazimika kula kama vile kula malisho ya wanyama, kuombaomba, kuuza mali zao ili kununua chakula. Mara nyingi wao ni masikini na ni wazi kuwa baadhi yao wanakufa kwa njaa,” 

Bwana Cirri ameongeza kuwa. “Njia pekee ya kukomesha njaa ni kuhakikisha usambazaji wa chakula kila siku na kwa wakati”.

Ameendelea kusema kuwa "Tumetaja hitaji la kujenga upya uwezo wa kujipatia riziki, kushughulikia sababu za msingi na kadhalika. Lakini iwe ni mara moja, kama kesho tunahitaji sana kuongeza usambazaji wetu wa chakula. Hii inamaanisha kusambaza msaada mkubwa na thabiti wa chakula katika hali ambayo inaruhusu wafanyikazi wa kibinadamu na vifaa kwenda kwa uhuru na kwa watu walioathiriwa kupata msaada huo kwa usalama."

Wanawke wakitembea kwenye maji ya mafuriko kwenye mji wa Johwar nchini Somalia
© WFP/Arete/Abdirahman Yussuf Mohamud
Wanawke wakitembea kwenye maji ya mafuriko kwenye mji wa Johwar nchini Somalia

Hatari nchini Sudan

Kuhusu Sudan, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa watu milioni 20.3 au asilimia 42 ya watu wote w anchi hiyo walitatizika kupata chakula cha kutosha mwaka jana, baada ya mzozo kuzuka mwezi Aprili.

Hii inawakilisha idadi kubwa zaidi ya watu duniani wanaokabiliwa na viwango vya "dharura vya uhaba mkubwa wa chakula, au daraja la nne, kulingana na kipimo cha tahadhari cha madaraja ya uainishaji wa uhakika wa chakula, ambapo daraja la tano (IPC5) linaonyesha kiwango cha juu cha hatari.

Huku zikiwa zimesalia wiki chache kabla ya msimu wa upanzi kuanza, msaada wa kibinadamu lazima uruhusiwe mara moja ndani na kote Sudan ili kuepuka kuzorota zaidi kwa hali hiyo, wamesisitiza waandishi wa ripoti hiyo.

Mabadiliko ya tabianchi na mdororo wa uchumi

Ripoti hiyo ambayo ni ushirikiano wa pamoja wa FAO, WFP na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF imetaja  sababu ya Pili ni matukio mabaya ya hali ya hewa yaliyochangiwa na mabadiliko ya tabianchi ambayo yamekuwa chanzo cha njaa katika nchi 18 na kuathiri kwa njaa zaidi ya watu milioni 77.

Na tatu mdororo wa kiuchumi uliokuwa chachu ya njaa katika nchi 21 na kuathiri jumlaya watu milioni 75.

FAO imesema kwa miaka minne mfululizo takriban asilimia 22 ya watu waliofanyiwa tathimini duniani wamekuwa wakikabiliwa na kutakuwa na uhakika wa chakula. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema “Mgogoro huu unahitaji hatua za haraka. Kutumia takwimu zilizoainishwa katika ripoti hii ili kufanyia marekebisho mifumo ya chakula na kushughulikia mizizi ya kutakuwa na uhakika wa chakula itakuwa muhimu sana”

Kwa mujibu wa ripoti waathirika wakubwa ni watoto, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mtandao wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa chakula imetoa wito wa haraka wa kubadili mtazamo ili ujumuishe amani, hatua za kuzuia na za maendeleo sambaba na juhudi za dharura kuvunja mzunguko wa janga la njaa ambalo linasalia katika viwango vya juu